NA DENIS MLOWE, MAFINGA
Mwanahabari Shalom Robert ametoa wito kwa Vijana kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika November 27 mwaka huu nchi nzima.
Aidha amewataka vijana kuacha tabia ya kulalamika kuhusu utendaji kazi wa viongozi wao na badala yake wafanye maamuzi sahihi ya kuwapigia kura Viongozi waadilifu na wachapakazi wanaofaa kuwa chachu ya maendeleo katika Mitaa, Vitongoji na Vijiji kwani kura za Uchaguzi ndizo zenye maamuzi ya kuwaweka madarakani viongozi wanaowahitaji.
Shalom Robert ambaye amekuwa mwanaharakati wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwa vijana aliyasema hayo wakati kama mgeni rasmi katika mchezo wa mpira wa miguu ulioambatana na zoezi la kuwahamasisha vijana na jamii kwa ujumla kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwapigia kura viongozi waadilifu na wanaofaa kwenye jamii.
Shalom alisema vijana wengi wamekuwa mstari wa mbele kulalamika kuhusu utendaji kazi wa baadhi ya viongozi kwenye maeneo yao lakini wamekuwa hawashiriki kwenye chaguzi na kupelekea baadhi ya viongozi wanaochaguliwa kukosa sifa.
‘vijana wengi tumekuwa na malalamiko sana juu ya baadhi ya viongozi kuwa hawafanyi kazi lakini ukiangalia hao hao vijana hawajitokezi kwenye chaguzi kuwapigia kura watu wanaowataka na kinachosalia ni lawama” amesema shalom.
Sambamba na hayo, Shalom, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi na kuwataka vijana kuendelea kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii sanjari na kupinga masuala ya uvunjifu wa amani kwa taifa la Tanzania.