Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, imefanikiwa kukamata kilo 2,207.56 za dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya katika operesheni zilizofanyika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam. Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema operesheni hizo zimepelekea kukamatwa kwa watuhumiwa saba.
Kamishna Lyimo alieleza Novemba 25, 2024, kwamba dawa zilizokamatwa ni pamoja na kilo 1,500.6 za skanka, kilo 687.76 za methamphetamine, kilo 19.20 za heroin, na chupa 10 za dawa aina ya Fentanyl. Aliongeza kuwa dawa hizi zingeweza kusababisha madhara makubwa endapo zingeingia mitaani, kwani zinaathiri sio tu watumiaji wa sasa bali pia huchochea kuanza kwa watumiaji wapya.
Matukio Muhimu ya Kukamatwa Kigamboni, Dar es Salaam (Novemba 14, 2024):Watuhumiwa Mohamed Bakari (40) na Sullesh Mhailoh (36), wote wakazi wa Mabibo, walikamatwa wakiwa na kilo 1,350.4 za skanka zilizofichwa kwenye nyumba iliyotumika kama ghala na gari aina ya Nissan Juke (T 534 EJC).
Sinza, Dar es Salaam (Novemba 14, 2024): Mtuhumiwa Iddy Mohamed Iddy (46), mkazi wa Chanika, alikamatwa akiwa na kilo 150.2 za skanka zilizofichwa kwenye maboksi ya sabuni na chasisi ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili wa Afrika Kusini (LN87XGP).
Tanga (Novemba 17, 2024):Watuhumiwa Ally Kassim Ally (52) na Fahad Ally Kassim (36) walikamatwa na kilo 706.96 za heroin na methamphetamine. Dawa hizo zilipatikana ndani ya gari aina ya Toyota Noah (T 714 EGX) na nyumba waliyopanga.
Kariakoo, Dar es Salaam (Novemba 19, 2024):M-Pes Watuhumiwa Michael Mziwanda (28) na Tumpale Mwasakila (32) walinaswa na chupa 10 za Fentanyl katika duka la M-Pesa
Katika operesheni hizo, DCEA pia ilikamata magari matatu na boti moja, ambavyo vilitumika kusafirisha dawa hizo. Vifaa hivyo viko chini ya ulinzi wa mamlaka hiyo kwa uchunguzi zaidi.
Kamishna Lyimo alisisitiza kuwa hatua hizi ni sehemu ya juhudi endelevu za DCEA kulinda jamii dhidi ya athari za dawa za kulevya. Alionya kuwa biashara ya dawa za kulevya inalenga makundi mapya ili kupanua soko, jambo ambalo linaongeza changamoto katika mapambano haya.
Operesheni hizi ni kielelezo cha dhamira ya DCEA kuhakikisha usalama wa afya ya jamii na kupunguza uhalifu unaochochewa na biashara ya dawa za kulevya.