Na: Mwandishi Wetu, Tanga.
Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ummy Mwalimu hatulii, hivi ndivyo unavyoweza kusema, baada ya kuambatana na wagombea mbalimbali wa nafasi za uenyeviti na wajumbe wao kutoka mitaa mbalimbali ya Tanga Mjini kuhakikisha wanaibuka kidedea katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotorajiwa kufanyia Novemba 27, 2024.
Novemba 23, 2024, Ummy Mwalimu ameshiriki mikutano minne kuwanadi wagombea wa mitaa ya Mabokweni (Kata ya Mabokweni), Ndumi (Kata ya Kiomoni), Putini (Kata ya Chongoleani) na Mleni (Kata ya Mzizima).
Ummy amewasihi wananchi kuwachagua wagombea hao walioaminiwa kupeperusha bendera ya CCM kwani hao ni wagombea sahihi, waliopikwa vyema na chama katika kuwatumikia wananchi.
Katika hatua nyingine, wagombea hao wameahidi endapo watapata ridhaa ya kuchaguliwa watachapa kazi kuhakikisha mitaa yao inapiga hatua kubwa za kimaendeleo.