Klabu ya Simba Sports Club imetoa wito kwa mashabiki wake kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tarehe 27, katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos.
Ahmed Ally, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, amesisitiza kuwa ushindi wa timu hiyo unategemea sapoti ya mashabiki wao. “Tiketi utakayonunua ni silaha muhimu ya kuisaidia Simba siku hiyo. Tunahitaji kuanza vizuri hatua ya makundi, na hili linawezekana tu kwa ushirikiano wa kila Mwanasimba,” alisema.
Akizungumza kuhusu siku hiyo ambayo pia itakuwa siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Ahmed Ally amewahimiza mashabiki kufanikisha majukumu yao ya kiraia mapema na kisha kuelekea uwanjani. “Ukishamaliza kupiga kura yako, elekea Uwanja wa Mkapa. Hakuna sababu ya Mwanasimba kukosa siku hiyo muhimu. Ushindi wetu unategemea nguvu za pamoja.”
Kwa upande wa maandalizi, Ahmed amebainisha kuwa klabu hiyo imejipanga kuwapa mashabiki furaha. “Tumejiandaa kuhakikisha kila Mwanasimba anayekuja uwanjani anaondoka na tabasamu. Tumepania msimu huu kila anayekuja lazima tumefunge. Jukumu letu ni kwenda uwanjani na kuhakikisha tunashangilia kwa nguvu,” alisisitiza.
Mgeni rasmi wa mchezo huo atakuwa ni Ahmed Ally mwenyewe, jambo ambalo limeongeza msisimko kwa mashabiki.
“Na mimi hapa ndiye nitakuwa mgeni rasmi katika mechi hii muhimu!” Ahmed Ally alihitimisha kwa tabasamu.
Mashabiki wa Simba sasa wanahimizwa kujitokeza kwa wingi na kuipa timu yao nguvu katika safari hii ya kuwania ubingwa wa Afrika.