Na Sophia Kingimali
Serikali kupitia Wizara ya Fedha imekitaka Chuo cha Kodi (ITA) kujikita katika tafiti zitakazosaidia kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa kodi na kuongeza kasi ya ulipaji wa kodi wa hiari.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alitoa wito huo leo, Novemba 22, 2024, jijini Dar es Salaam, wakati wa mahafali ya 17 ya Chuo cha Kodi, ambapo jumla ya wahitimu 417 walitunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa Chuo cha Kodi katika kutoa mafunzo ya kodi na forodha, kwani mafunzo hayo yanachangia kuongeza mapato ya kodi kwa Taifa,” alisema Mwandumbya.
Alihimiza chuo hicho kuendelea kutoa mafunzo ya viwango vya juu kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia, akisisitiza kuwa tafiti zinazolenga changamoto za ukusanyaji wa kodi ni muhimu kwa kufikia malengo ya Taifa.
Aidha, aliwataka wahitimu kuwa mabalozi wa elimu ya ulipaji kodi popote walipo, huku akitoa wito kwa sekta binafsi kuajiri wataalamu wa kodi ili kuongeza uelewa na motisha ya ulipaji wa kodi kwa hiari.
Mkuu wa Chuo cha Kodi, Prof. Isaya Jairo, alisema kuwa chuo hicho kimefanikiwa kuzalisha wataalamu wenye umahiri katika masuala ya forodha na kodi, wakilenga kukuza uchumi wa Taifa kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa.
“Tumetoa mafunzo ya mkakati kwa wafanyakazi 7,438 hadi sasa, kuhakikisha wanakuwa na ujuzi wa kukabiliana na changamoto za ukusanyaji wa kodi,” alisema Prof. Jairo.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, alieleza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuboresha miundombinu ya chuo hicho ili kuhakikisha kinazalisha wahitimu bora kwa maendeleo ya nchi.
“Pia tunaangalia uwezekano wa kupanua mafunzo ya lazima kwa wafanyakazi wa ngazi za juu kama sehemu ya mkakati wa kuongeza idadi ya walipa kodi na kuimarisha ulipaji wa kodi,” aliongeza Mwenda.
Mahafali hayo yameonesha umuhimu wa Chuo cha Kodi katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia elimu bora na tafiti zinazolenga kuboresha mfumo wa kodi nchini.