RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisaini hati ya makubaliano ya Mpango wa Maboresho ya Utoaji wa Huduma Bandari ya Zanzibar (Zanzibar Port Improvement) hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo 22-11-2024.(Picha na Ikulu)
WAGENI Waalikwa na Viongozi mbalimbali wa Taasisi za Serikali wakifuatilia hafla ya utiaji wa Saini wa Mpango wa Maboresho ya Utoaji wa Huduma wa Bandari ya Zanzibar (Zanzibar Port Improvement) wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo 22-11-2024.(Picha na Ikulu)
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla na (kulia kwake) Muwakilishi wa Taasisi ya Tony Blair. Sydney Chibbabbuka na viongozi wa Serikali wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia wakati wa hafla ya utiaji wa Mpango wa Maboresho ya Huduma za Bandari Zanzibar (Zanzibar Port Improvement) uliofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo 22-11-202.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Utiaji wa Saini wa Mpango wa Maboresho ya Utoaji wa Huduma Bandari ya Zanzibar (Zanzibar Port Improvement) uliofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo 22-11-2024.(Picha na Ikulu)
IKULU – ZANZIBAR,
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amebainisha mikakati ya Serikali juu ya ukuaji uchumi wa Zanzibar na kueleza kuwa inaendelea kuwawekea mazingira rafiki ya biashara wafanyabiashara wote wanaotumia bandari ya Zanzibar.
Dk. Mwinyi amesema hayo alipozindua, kusaini na kushuhudia utiwaji wa saini Mpango wa maboresho ya utoaji huduma kwa bandari ya Zanzibar (Zanzibar Port Improvement Charter) kwa ushirikiano wa Serikali, wadu wa bandari kutoka taasisi za umma na binafsi pamoja na Taasisi ya Tony Blair (TBI), hafla iliyofanyika viwanja vya Ikulu, Zanzibar.
Amesema, lengo la mpango huo ni kuondosha usumbufu kwa kupeana majukumu kwa kila mdau, kupitia viashiria vilivyoandaliwa ndani ya mpango huo sambamba na kurahisisha ushushaji wa makontena (Makasha), ukaaji wa meli ukutani, kusubiria ukuta pamoja masuala ya ‘Customes Clearance’ kwa kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za bandari ili kutoa msukumo wa ukuaji wa Uchumi wa nchi.
Akizungumzia suala la upakiaji na ushushaji wa Makontena bandarini, Rais Dk. Mwinyi amewahakikishia wafanyabiasha wa Zanzibar kwamba Serikali imedhamiria kwa dhati kuimarisha utoaji wa huduma kwa kurahisisha mchakato wa upakiaji na ushushaji wa kontena (Makasha) katika Bandari zote nchini.
Alisema, hatua hiyo ni kwa mujibu wa wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 katika Ibara ya 167(b) inayozungumzia Kuimarisha huduma za bandari kwa kutumia vifaa na teknolojia za kisasa ili kuongeza idadi ya makontena (TEUs) kutoka 82,312 mwaka 2018 hadi makontena 105,000 ifikapo 2025 pia kupunguza idadi ya siku za kuegesha meli kutoka siku saba mwaka 2018 hadi siku tano mwaka 2025 ambayo kwa sasa uwezo wa bandari za makasha tatu; Malindi, Fumba na Mkoani Pemba zina uwezo wa kuhudumia makasha zaidi ya 105,000.
Aidha Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa makubalianao hayo baina ya Serikali na taasisi hizo ni utekelezaji na ufanisi kwa Babdari ya Zanzibar pia kutafanyika upimaji wa kila kilichotekelezwa na taasisi hizo kila inapotimia mwaka mmoja.
Alitanabahisha kwamba endapo taasisi zote zitatekeleza wajibu wao ipasavyo, mafanikio makubwa yatapatikana nchini, akitolea mfano nchi za Singapore, Mombasa – Kenya, Gambia kwa kufanikiwa na mpango kama huo wa utoaji huduma wa bandari ambao wamepiga hatua kubwa ya mafanikio.
Katika hatua nyengine ya kuboresha huduma za bandari Rais Dk. Mwinyi amesema, Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa Bandari jumuishi ya Mangapwani inayotarajiwa kuhudumia meli kubwa za mafuta na gesi. Alieleza ujenzi wa bandari hiyo unakwenda sambasamba na ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM, kifungu 167(c) kinachoielekeza Serikali kujenga miundombinu ya kuhudumia meli zinazopita mwambao wa Afrika Mashariki, kupata huduma za kuongeza mafuta, maji safi na kufanya matengenezo.
Hata hivyo, Dk. Mwinyi aliwataka wadau wa bandari ya Zanzibar ikiwemo Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi yenye kubeba jukumu kubwa la Taifa, la kusimamia miundombinu nchini, kuendelea kuwa karibu na watumiaji wa miundombinu hiyo kwa kuwapelekea huduma na nyenzo ili kuhakikisha wananchi wanatumia miundombinu bora na yenye tija kwa ustawi wa jamii na kuinua uchumi wa Zanzibar kwa maendeleo ya wananchi.
Vile vile, Rais Dk. Mwinyi ameeleza jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi wanashirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza sekta ya Uchukuzi.
Akibainisha miongoni mwa harakati hizo ni kuimarisha miundombinu ya barabara pamoja na bandari kwa Unguja na Pemba ili kuwarahisishia huduma wanachi na wafanyabiashara.
Pia, aliwaomba wafanyabiashara waendelee kufanya kazi zao kwa uaminifu, maadili na uzalendo ili kujipatia kipato halali na kuzingatia wajibu wao wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Akizungungumza kwenye hafla hiyo, Waziri Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed amesema kusainiwa kwa Mpango huo wa maboresho ya utoaji wa huduma za Bandari ya Zanzibar ni makubaliano baina ya Serikali na wadau wa bandari hiyo zikiwemo taasisi za Umma na binafsi kufanyakazi kwa pamoja ili kuongeza ufanisi na kuleta tija katika kukuza Uchumi wa nchi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Akif Ali Khamis amepongeza hatua ya Serikali kuleta Mapinduzi makubwa kwa sekta ya bandari ya Zanzibar juu ya uendeshaji wa bandari hiyo baada ya kuingia mkataba na Kampuni za Zanzibar Multiple, kampuni ya Bandari ya Fumba na ya Mkoani kwaajili ya kushusia makasha (makontena.
Alisema, tokea kuanza maboresho yaliyosimamiwa na Kampuni ya Zanzibar Multiple amesifu mafanikio makubwa yalitofikiwa na bandari hiyo ikiwemo kupungua siku za kusubiri meli kutoka siku 40 hadi 20 hadi kufikia siku nane kwa mara ya kwanza kutokea kwa bandari hiyo akisifu ufanisi wa kuhudumia meli kuongezeka. Pia ametoa wito kwa wadau wa huduma badari hiyo, wabadilike na hatimae waendane na ushindani wa bandari uliopo hivi sasa ulimwenguni.
Kwa upande wake kiongozi wa timu ya Taasisi ya Tony Blair, Frank Matsaert amesifu juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuusimamia hadi kuufanikisha mpango huo na kueleza kwamba utakwenda kufungua mafanikio ya ukuaji wa Uchumi wa Zanzibar kupitia lango la Bandari hiyo.