Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua kampeni mpya iitwayo “WALETE,” ikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini. Kampeni hii inalenga kuwafikia wateja wote, mijini na vijijini, kwa kuwapa vifurushi bora, nafuu, na vinavyokidhi mahitaji ya mawasiliano ya kidijitali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, alisema kuwa kampeni ya “WALETE” inalenga kuleta suluhisho la mawasiliano linalozingatia thamani na mahitaji ya wateja. “Lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za mawasiliano zinazokidhi mahitaji yao, huku tukizingatia urahisi wa upatikanaji na gharama nafuu,” alisema Mwita.
Kampeni hiyo imejikita pia katika kuboresha vifurushi maarufu vya TTCL, ikiwa ni pamoja na:
Jiachie Xtraa: Kifurushi hiki kinampa mteja uhuru wa kuwasiliana kwenda mitandao yote bila ukomo wa muda.
T-Connect Plus: Kinajumuisha muda wa maongezi, ujumbe mfupi (SMS), na intaneti kwa bei nafuu.
Bufee Tena: Kifurushi hiki kinamruhusu mteja kuchagua kiwango cha huduma anachotaka, ikijumuisha Dakika, SMS, au Data kulingana na mahitaji yake.
Kwa mujibu wa Mwita, TTCL pia imeimarisha upatikanaji wa vocha kwa njia za kidijitali kupitia T-Pesa, benki kama CRDB na NMB, pamoja na mitandao mingine ya simu. Hii inalenga kurahisisha ununuzi wa vifurushi bila kuhangaika.
Balozi wa kampeni hiyo, Clayton Chipando, maarufu kama Baba Levo, alisisitiza ubora wa mtandao wa TTCL, hasa katika utoaji wa huduma za intaneti. “Mtandao wa TTCL ni bora zaidi, na ndio chaguo sahihi kwa Mtanzania anayetaka kuperuzi kwa haraka na kwa gharama nafuu,” alisema Baba Levo.
Kwa kampeni hii, TTCL inalenga si tu kuboresha mawasiliano lakini pia kuimarisha ushindani kwenye soko kwa kutoa huduma zinazowagusa moja kwa moja wananchi wa kawaida. TTCL imedhamiria kuleta mapinduzi katika mawasiliano nchini kupitia teknolojia ya kisasa na huduma bora zaidi.