Meneja mradi wa ujenzi wa meli ya Mv.Mwanza, Mhandisi Vitus Mapunda (Kulia) akitoa taarifa ya mradi huo kwa mratibu wa kongamano la vijana na Tanzania Lazaro Nyarandu.
Mhandisi wa umeme na mitambo kwenye meli ya Mv.Mwanza, Felix Kitambi (katikati) akitoa maelekezo kwa mratibu wa kongamano la vijana na Tanzania Lazaro Nyarandu.
Mratibu wa Kongamano la Vijana na Tanzania, Lazaro Nyarandu akizungumzia mradi wa meli ya Mv Mwanza utakavyoleta fursa kwa vijana.
Mratibu wa Kongamano la Vijana na Tanzania, Lazaro Nyarandu (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na vijana baada ya kumaliza kutembelea meli ya Mv Mwanza katika Bandari ya Kusini Jijini Mwanza.
…….
Na Hellen Mtereko, Mwanza.
Vijana wametakiwa kuchangamkia fursa katika miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini hatua itakayowasaidia kupata ajira.
Hayo yamebainishwa Leo Jumanne 20, 2024 na Mratibu wa Kongamano la Vijana na Tanzania, Lazaro Nyarandu wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali jijini Mwanza akiwa ameambatana na vijana 50 wenye kaulimbiu isemayo “Samia Love”
Akizungumza mara baada ya kukagua meli ya Mv. Mwanza inayojengwa katika Bandari ya Kusini Jijini hapa, Nyarandu alisema vijana wasisubili meli hiyo izinduliwe ndio waanze kutafuta kitu cha kufanya badala yake waanze kufikiria vitu ambavyo watauza katika maeneo ambayo meli hiyo itaenda.
“Vijana wanatakiwa kubuni na kuthubutu kutumia fursa ya meli hii hata kabla ya kuanza kufanya kazi ili ikianza kazi rasmi wawe tayari na mipango endelevu itakayowasaidia kujiari,meli hii itabadilisha maisha ya watu wengi na itakuwa na tija kwetu sisi na nchi jirani “, alisema Nyarandu.
Aidha, Nyarandu alitumia fursa hiyo kuwakaribisha vijana wote wa mkoa wa Mwanza na mikoa jirani kushiriki kwenye Kongamano la Vijana na Tanzania kwakushirikiana na Samia Love litakalofanyika Novemba 22, 2024 katika Wilaya ya Ilemela Jijini hapa.
Kwaupande wake mmoja wa vijana aliyeambatana na Mratibu wa Kongamano hilo, Catherine Mwasulama alisema wao kama vijana wanatakiwa kuachana na tabia ya kuilaumu Serikali kwamba haitoi ajira badala yake wafikirie katika kujiajiri wenyewe.
“Sisi kama vijana hatupaswi kuwa na lawama tujiulize sisi tutaifanyia nini inchi yetu kwani kijana ni nguvu kazi ya Taifa pia ni mtaji”, alisema
Alisema mradi wa meli ya Mv. Mwanza utakapokamilika utawasaidia vijana kupata ajira zitakazowaongezea kipato.
Awali akitoa tariafa ya ujenzi wa meli ya Mv. Mwanza Meneja mradi wa meli hiyo, Mhandisi Vitus Mapunda alisema ujenzi umefikia asilimia 98 na ina urefu wa mita 92 na upana wa mita 17.