Serikali ya Tanzania imejipanga katika kuhamasisha zao la mimea aina ya bamboo (mianzi) katika kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamejiri wakati wa mjadala wa Bamboo kando mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) unaoendelea jijini Baku nchini Azerbaijan leo Novemba 19, 2024.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, Mkurugenzi Masoko wa Bodi ya Utali Tanzania (TTB) Bw. Ernest Mwamwaja amesema mimea inayolengwa ina uwezo wa kunyonya hewa ukaa kwa haraka na kupunguza majanga ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa ardhi na mafuriko.
Bw. Mwamwaja amefafanua kuwa mmea wa bamboo pamoja na mambo mbalimbali pia hutumika katika ujenzi, kutengeneza samani mbalimbali, vifungashi na vinywaji.
Mjadala huo umefanyika mbele ya Viongozi wa Mtandao wa Bamboo Duniani (INBAR) na wadau wengine wanaohusika na usainishaji Mkataba kati ya INBAR na UNFCCC kuhusu uendelezaji wa zao la bamboo kwa ajili ya kuhimili mabadiliko ya Tabianchi.
Aidha, wadau wote katika mkutano huo wamekubaliana kuhakikisha NDC inatambua zao hilo na upatikanaji wa fedha kupitia maandiko na biashara ya kaboni.
Halikadhalika, wadau wamekubaliana kuendelea kujenga uwezo wa wadau kuhusu zao hili katika kuhimilia athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili Tanzania na dunia kwa jumla.
Itakumbukwa kuwa kwa sasa bamboo ni zao ambalo linahamasishwa kupitia Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Bamboo wa mwaka 2023 hadi 2030.
Mkutano huo uliwahusisha pia maafisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na sekta mbalimbali.