*Kila wilaya kupatiwa mitungi ya gesi 3,255
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogoro ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuingia mkataba na mtoa huduma kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited ambaye atahudumia wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Mbeya kwa kuuza kwa bei ya ruzuku mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Mpogoro ametoa pongezi hizo leo Novemba 20, 2024 mkoani humo baada ya uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ugawaji mitungi ya gesi ya uzito wa kilo sita iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala, Mha. Advera Mwijage.
Mpogoro amesema kuwa mitungi ya gesi itakayosambazwa mkoani Mbeya itachochea kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi na salama.
“Naipongeza REA kwa kuja na mradi huu, naiomba iwe endelevu ili iweze kuwasambazia wananchi wengi nishati hii muhimu itakayokuwa mkombozi kwetu, ” amesema Mpogoro.
Mha. Mwijage amesema, Serikali kupitia REA imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi (LPG) katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa mji.
“Lengo la mradi ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti ambapo takribani hekta 400,000 hukatwa kila mwaka, ” Ameongeza Mha. Mwijage.
Amezitaja wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja na Wilaya ya Mbeya, Chunya, Kyela, Mbarali na Rungwe