Na Sophia Kingimali
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 17 ya Chuo cha Kodi (ITA) yatakayofanyika Novemba 22, 2024, katika kampasi ya chuo hicho, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 20, 2024, Mkuu wa Chuo cha Kodi, Isaya Jairo, alieleza kuwa Waziri Mwigulu atatunuku vyeti vya stashahada, shahada, na stashahada ya uzamili kwa jumla ya wahitimu 417 wa mwaka wa masomo 2023/2024.
“Kati ya wahitimu hao, wanafunzi 236 ni wa kiume na 181 ni wa kike. Aidha, wanafunzi 195 watatunukiwa Cheti cha Uwakala wa Forodha cha Afrika Mashariki (EACFFPC), wahitimu 28 watapokea Cheti cha Usimamizi wa Forodha na Kodi (CCTM), na wanafunzi 61 watatunukiwa Shahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi (DCTM),” alisema Jairo.
Sambamba na shughuli ya kutunuku vyeti, Waziri Mwigulu pia atatoa zawadi kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wamefanya vizuri katika mwaka wa masomo 2023/2024.
Pia, chuo kitatambua wafadhili waliochangia maendeleo ya elimu kwa kutoa machapisho na nyenzo mbalimbali muhimu kwa wanachuo.
Mahafali haya yanatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya kodi na forodha, pamoja na familia za wahitimu, ikiwa ni hatua muhimu ya kuadhimisha mafanikio ya kielimu na kitaaluma ya wanafunzi wa ITA.