Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,Missaile Musa akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa wataalamu wa manunuzi na Ugavi mkoani Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi hapa nchini(PSPTB)Godfred Mbanyi akizungumza kwenye semina hiyo inayoendelea mkoani Arusha.
………..
Happy Lazaro,Arusha .
WATAALAMU wa ununuzi na Ugavi nchini wametakiwa kuwa waadilifu na weledi katika utendaji kazi wao huku wakitanguliza uzalendo pamoja na kuzingatia kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku .
Hayo yamesemwa leo mkoani Arusha na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,Missaile Musa wakati akifungua mafunzo kwa wataalamu wa manunuzi na Ugavi ambayo yameandaliwa na Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi(PSPTB)na kushirikisha wataalamu wa sekta hiyo toka halmashauri zote na sekretarieti ya mkoa wa Arusha.
Aidha amewataka kuzingatia misingi ya taaluma yao kwani taaluma hiyo ya ununuzi na Ugavi ni kubwa sana na lazima waitendee haki kwa kufuata maadili ya kazi hiyo na kuweza kuwa mfano wa kuigwa.
“Kupitia mafunzo haya kutasaidia sana kukumbushwa wajibu wenu kuhusu michakato ya manunuzi ili ipatikane bila ucheleweshaji kwani nimeambiwa kuwa mtaweza kujifunza sheria mpya ya ununuzi na Ugavi ambayo inaelekeza weledi na usimamizi wa fedha za serikali. “amesema .
Aidha Musa amewataka kujiepusha na vitendo vya rushwa na kujikita zaidi katika kusimamia kikamilifu fedha zote za umma zinazotengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali.
“hakikisheni mnajifunza kwa umakini mkubwa kuandaa na kutunza mikataba,na mzingatie yaleyote mnayofunzishwa hapa ili mkitoka muende mkayatekeleze kwa vitedo”alisisitiza katibu Tawala huyo wa Mkoa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi hapa nchini(PSPTB)Godfred Mbanyi amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wataalamu hao juu ya sheria mpya ya ununuzi na namna ya kusimamia mikataba.
Amesema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo katika maeneo mengi hapa nchini ni wataalamu wa ununuzi kufanya kazi pasipo kusajiliwa na bodi hyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kuwataka wale wote ambao hawajasajiliwa wajisajili mara moja.
“Natoa wito kuzingatia sheria kanuni na taratibu za manunuzi katika kutekeleza majukumu yenu,na nawataka wale wote ambao hawajasajiliwa na bodi kujisajili haraka iwezekanavyo kwani iko kwa mujibu wa sheria na anayefanya kazi bila kusajiliwa anavunja sheria za nchi”amesema Mbanyi.
Kwa upande wake Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo,Catherine Mwamasage ambaye ni Mkuu wa kitengo cha manunuzi kutoka TANAPA,amepongeza PSPTB kwa kuwapatia mafunzo hayo na kusema kuwa yatawasaidia kupata maarifa zaidi na wataenda kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Aidha mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi(PSPTB)na kushirikisha wataalamu wa sekta hiyo toka halmashauri zote na sekretarieti ya mkoa wa Arusha.