Halmashauri ya mji wa Njombe imekiri kuweka sawa mazingira ya uchaguzi wa serikali za mitaa hadi kwa makundi maalumu ili yaweze kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hapo Novemba 27 mwaka huu.
Mbele ya Vyombo vya Habari Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya mji wa Njombe Kuruthum Sadick ambaye ni mkurugenzi wa Halmashauri hiyo amesema kila kitu kipo sawa kuanzia kuzinduliwa kwa Kampeni hapo Kesho[Hii Leo] na kwamba makundi maalumu yatapewa kipaumbele siku ya Kupiga kura.
Aidha Kuruthum Sadick amevitaka vyama vya siasa vya CCM na CHADEMA Vinavyoshiriki uchaguzi huo pamoja na wagombea kufuata kanuni na taratibu kwa mujibu wa Sheria na makubaliano katika uendeshaji wa Kampeni.
Kwa upande wao wananchi mkoani Njombe akiwemo Seif Mtamike,Deus Sanga na Rejino Mwapinga wamesema hawataki sera za uongo kwa wagombea ambazo hazitekelezeki.
Kituo hiki kimezungumza na Vyama vya siasa kwa njia ya Simu kutaka kujua namna vilivyojipanga katika Kampeni na Wagombea wao ambapo Katibu wa Siasa na uenezi CCM Mkoa wa Njombe Josaya Luoga anasema kila jimbo limeweka utaratibu wa kuzindua kampeni
Naye Katibu wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Njombe Stanley Mbembati anasema watashiriki katika Kampeni hizo mwanzo hadi mwisho licha ya wagombea wao wengine kutorejeshwa hususani Katika Jimbo la Njombe mjini ambalo hakuna mgombea hata mmoja aliyerejeshwa.
Baraka Kivambe ni Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Ambaye anakiri kurejeshwa kwa wagombea wao kwa kiasi kikubwa na wako tayari kushiriki kikamilifu katika Kampeni hizo.
Novemba 26 Kampeni hizo zitatamatika na Novemba 27 kufanyika kwa uchaguzi wa kuwapata wenyeviti wa Mitaa,Vijiji,Vitongoji na Wajumbe wa Serikali za Mitaa.