Na Mwandishi Wetu – SONGWE
Mahakama ya Wilaya ya Songwe imemhukumu Assan Jacob Kalinga, aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Mbuyuni katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la uhujumu uchumi.
Hukumu hiyo imetolewa mnamo Novemba 18, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mh. A. Lugome, kufuatia kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2023. Kalinga alitiwa hatiani kwa ufujaji wa fedha za umma kiasi cha Tsh. 7,721,000/-, fedha zilizokuwa zimekusanywa na wananchi wa Kijiji cha Mbuyuni kwa ajili ya ununuzi wa mita za umeme wa REA kati ya mwezi Aprili hadi Oktoba 2020.
Kesi hiyo iliendeshwa na Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, Bi. Simona Mapunda, ambaye alithibitisha kuwa mshtakiwa alivunja Kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, sura ya 329, pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza na Kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, sura ya 200.
Katika hukumu yake, Mh. Lugome alibainisha kuwa ubadhirifu wa fedha hizo sio tu ulikwamisha mradi wa kijiji, bali pia ulikiuka maadili ya uongozi na kuathiri maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa TAKUKURU mkoa wa Songwe, adhabu hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha viongozi wa umma wanawajibika na kuepuka vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
“Hii iwe fundisho kwa viongozi wengine wanaotumia madaraka yao vibaya. TAKUKURU itaendelea kusimamia haki na uwajibikaji,” alisema Bi. Mapunda baada ya hukumu hiyo.
Kifungo cha miaka 20 kwa Assan Kalinga kinaashiria msimamo mkali wa vyombo vya sheria dhidi ya makosa ya uhujumu uchumi nchini.