Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Uongozi wa Wilaya ya Pangani umepokea agizo la kuhakikisha kwamba, bati zote zilizokosa kukidhi viwango vya ubora kutoka Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) na kuezekwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo, ziondolewa na zifanyiwe mabadiliko kwa bati mpya.
Aidha, wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga wametakiwa kuwa waaminifu katika usambazaji wa vifaa vya ujenzi kwenye miradi ya Serikali ili kuepuka ubora duni wa vifaa katika miradi muhimu.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdurahman Abdallah, alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la hospitali kongwe ya Wilaya ya Pangani, mradi uliopewa fedha na Serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.
Katika ziara hiyo, Ustaadh Rajabu alisisitiza kuwa ni jukumu la Chama Cha Mapinduzi (CCM), chenye Ilani inayotekelezwa, kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi inayopokea fedha za Serikali ili kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika ipasavyo.
“Kama Chama, ni wajibu wetu kuhakikisha fedha zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kama ilivyokusudiwa. Hivyo, tunatembelea miradi ili kujionea maendeleo yake,” alisema Ustaadh Rajabu.
Akizungumzia suala la bati zilizokosa ubora katika hospitali hiyo, Ustaadh Rajabu alisema kuwa waligundua tatizo hilo na kutoa maelekezo kwa uongozi wa wilaya kuhakikisha bati hizo zinabadilishwa mara moja ili kuzingatia viwango vya TBS.
“Mimi nasisitiza tena, ni lazima bati hizi zote ziondolewe na zielekezwe bati zinazokidhi viwango ili kuhakikisha mradi huu unaendelea kwa ubora na manufaa kwa wananchi,” alisema.