Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) amefanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara leo tarehe 18 Novemba, 2024 jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo ya viongozi hao yameangazia ushirikiano wa kihistoria na wa kidiplomasia baina ya Tanzania na China ambapo wameahidi kuendelea kuimarisha na kukuza ushirikiano uliopo kwa maslahi ya pande mbili.
Mhe. Chumi ameeleza kuwa Tanzania inafurahishwa na hatua za ushirikiano zilizofikiwa hususan kwa nchi hizo mbili kuwa na ziara za viongozi wa ngazi za juu ambazo zimeendelea kustawisha ushirikiano na kuweka mikakati mbalimbali ya kukuza ushirikiano huo.
‘’Tunashukuru kwa ushirikiano mnaotupa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu hususan maboresho ya ujenzi wa reli ya TAZARA ambayo ni kiungo muhimu katika kuiunganisha Tanzania na nchi jirani ambazo hutumia bandari ya Dar es Salaam’’, alisema Mhe. Chumi.
Miradi mingine ni ukamilishaji wa daraja la Magufuli mkoani Geita ambalo likikamilika litaondoa changamoto ya usafiri kwa wakazi wa mkoa huo pamoja na kuruhusu shughuli za maendeleo hususan biashara.
Naye Mhe. Mingjian ameeleza kuwa ushirikiano wa Tanzania na China umekuwa na matokeo chanya kwa pande zote mbili ambapo ameeleza katika miaka 60 ya ushirikiano Serikali ya China imefuta tozo kwa Tanzania kuingiza mazao ya kilimo nchini humo.
‘’Ni vema watanzania wakatumia fursa hiyo kunufaika kiuchumi kupitia jitihada zinazofanywa na Serikali, kwakuwa fursa hii haijatolewa kwa nchi zote isipokuwa kwa nchi chache ikiwemo Tanzania kufuatia mkakati wa kipaumbele unaotolewa na China’’, alihamasisha Mhe. Mingjian.
Pamoja na masuala mengine, utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa kilele wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba, 2024 Beijing, China ilikuwa sehemu ya ajenda muhimu ya mazungumzo ya viongozi hao.