Mkuu wa Chuo Cha Biblia Cha Kilutheri Nyakato Meanza,Mimii Mziray akizungumza kwenye mahafali ya 13
Wahitimu wa chuo Cha Bibilia wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi.
Wahitimu wa Chuo Cha Biblia Cha Kilutheri Nyakato Jijini Mwanza wakiwa kwenye maandamano.
………
Na Hellen Mtereko, Mwanza.
Wahitimu wapya 39 wa fani za uchungaji (theolojia), uinjilisti na wasaidizi wa usharika wametakiwa kuikomboa jamii iliyotumbukizwa kwenye mahubiri potoshi yanayoikabili jamii ya Watanzania kwa sasa na kuepuka kufuata mkumbo wa tamaa ya utajiri na kuwatoza waumini fedha nyingi kama ilivyo kwa baadhi ya manabii wengi mtaani.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi Novemba 16, 2024 na Askofu mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki Ziwa Viktoria, Oscar Lema wakati akihitimisha mahafali ya 13 ya Chuo cha Biblia cha Kilutheri Nyakato, Mwanza, lengo likiwa ni kuikomboa jamii inayoteswa na changamoto mbalimbali kutokana na utitiri wa wahubiri wasio na sifa.
Amesema walimu wengi walio mtaani ni wale ambao hawajapata mafundisho sahihi ya neno la Mungu, hivyo matarajio ya kanisa hilo kuona wahitimu hao wanakuwa mbegu itakayoleta matunda mema kwa kuikomboa jamii iliyotumbukia kwenye upotoshaji na kuwa baraka huko waendako kwa kuhubiri neno la Mungu na kulisimamia kwa usahihi.
“Wananchi wanahitaji chakula habari njema za uokovu siyo Nyakato wala historia yenu na habari za upotoshi, watu wana changamoto wanataka majibu yake na wakristu ndiyo watoa maksi. Mujiongeze muwe na maarifa makubwa ya neno la Mungu na mambo mengine ili kuendana na mazingira ya sasa na kuwasaidia,” amesema Askofu Lema
“Tutarajie kwamba neno la Mungu linahuburiwa kwa usahihi na mtakuwa watu ambao watapinga na watasimamia neno la Mungu kwa usahihi. Tunachowatakia ni baraka za Mungu lakini mwende mkafundishe sawa sawa na kile wasimame katika hayo na wasifuate yale ambayo watayakuta huko,” amesema
Mkuu wa Chuo cha Biblia Kilutheri Nyakato, Mimii Mziray amewataka wahitimu hao ambao ni watenda kazi wasivutwe na mafundisho ambayo yanalenga kujinufaisha wao wenyewe kwani wana nafasi kubwa katika maisha ya watu, huku akiahidi chuo hicho kuboresha mitaala yake ili kutoa huduma nzuri kwa jamii na inayoendana na wakati wa sasa.
“Tunatakiwa kutenda mema, kupenda haki na kutenda rehema na kutembea kwa unyenyekevu. Maadili haya ni muhimu katika utumishi wenu kiroho na itawasaidia kuwa mashahidi wa kweli wa Yesu Kristo, msiache kuendelea kujifunza, kukua na kuwa mfano bora kwa sharika zenu,” amesema Mziray
Mhitimu wa Astashahada ya Theolojia, Ezekiel Kamkuru amekiri jamii kuwa njia panda kutokana na kuibuka kwa wahubiri ambao hawana elimu sahihi ya neno la Mungu huku akiahidi kuyatumia mafunzo hayo kuinjilisha na kuwasaidia watu kukabiliana na changamoto za kimwili na kiroho ili kuwatafuta walio gizani kuwaonyesha nuru ili waifahamu kweli.
Naye, Martha Maboya, Mteolojia amesema “Naamini kupitia mafundisho yetu tutawasaidia watu kusimamia katika neno la Mungu. Mchungaji anapaswa kuwahudumia watu siyo wao ndiyo wamhudumie hatutakiwi kuvutwa na mafanikio tunayoyaona watu wengine huko mtaani,”
Kaimu Mkuu wa Kitivo cha Theolojia Chuo Kikuu cha Iringa, Dk Lincoln Kimiliki akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edward Hosea amesema kutokana na uwepo wa mambo yanayoleta utata katika jamii, wahitimu wa theolojia kwenye vyuo vya kanisa hilo washirikiane katika uboreshaji wa elimu hiyo ili kupata majibu ya mambo hayo.
“Jamii yetu imekumbwa na mazingira yanayobadilika sana jambo hili linadai elimu ya Theolojia ibadilike ili kuendana na mazingira hayo iwe na ubora endelevu. Tuongeze kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika ufundishaji ili kutoa elimu inayowajengea wahitimu kutoa huduma inayokubalika katika maeneo watakayopangiwa kuhudumia,” amesema Dk Kimiliki
Ameoongeza kuwa “elimu siyo mali yako ni sharti itumike kwa watu na kuleta matunda mema. Elimu hai inakuwa ni mkombozi kwa wananchi wengi hususan walio kwenye mateso ya upotoshaji, tuendelee kujitathmini namna tutakavyotumia elimu tuliyoipata kuongeza tija katika maeneo tunayokwenda,”
Katika mwaka wa masomo 2023/2024 jumla ya wanafunzi 39 wamehitimu chuoni hapo katika kozi za Teolojia, Uinjilishaji na wasaidizi wa usharika, wanafunzi 13 wamehitimu Astashahada ya Theolojia na wengine 18 wakitunukiwa cheti cha Uinjilisti na mwanafunzi mmoja akihitimu msaidizi wa usharika (Parish Worker) kutoka Chuo cha Biblia Nyakato. Wahitimu watano wametunukiwa Astashahada ya Theolojia kutoka Chuo Kikuu cha Iringa huku wawili wakitunukiwa Stashahada ya chuo hicho.