NA MWANDISHI WETU
MAAFANDE wa timu za Kikosi cha Kuzuia Magendo KMKM wanawake na wanaume wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi ya Kabaddi ‘Season One’, baada ya kushinda katika michezo yao ya fainali iliyochezwa kwenye kiwanja cha nje New Amaan Complex.
KMKM wanawake walishuka dimbani majira ya saa 8:00 mchana na kufanikiwa kuifunga timu ya Lumumba kwa pointi 41-18, huku KMKM wanaume wakishuka majira ya saa 10:00 na kuifunga Bububu Kabaddi kwa pointi 101-34.
Kiujumla fainali zote mbili zilionesha ushindani wa hali ya juu na kutoa burudani tosha machoni mwa mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo.
Katika fainali hizo mgeni rasmi alikuwa ni Katibu wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan ambae alikabidhi zawadi za vikombe kwa washindi hao.
Mabingwa hao na washindi wa pili walikabidhiwa vikombe huku mshindi wa tatu kwa wanaume ambae ni timu ya King Warriors Kabaddi kukabidhiwa kikombe kidogo.
Jumla ya timu tisa zilishiriki ligi hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika tokea Shirikisho la mchezo huo kupata usajili, zikiwemo timu tano za wanaume na nne za wanawake.
Timu hizo kwa upande wa wanaume ni KMKM, Bububu, Lumumba, K. Warriors na wanawake ni KMKM, Lumumba, K. Worriors na Bububu.