Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Adam Mihayo akiwasilisha maelezo kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali PAC wakati wanumbe wa kamati hiyo ilipotembelea makao makuu ya benki ya TCB kinitonyama jijini Dar es salaam Leo Novemba 16, 2024.
Mwenyekiti wa Kamati, Augustino Vuma wakati kamati hiyo ilipotembelea makao makuu ya benki ya TCB kinitonyama jijini Dar es salaam Leo Novemba 16, 2024.
……………..
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam: Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwezeshaji Taasisi za Umma imeonesha kuridhishwa na utendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), huku ikiitaka benki hiyo kuendelea kutoa gawio kwa Serikali Kuu ili kuchangia utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayowanufaisha Watanzania.
Akizungumza leo wakati wa ziara ya kamati hiyo katika ofisi za TCB, Mwenyekiti wa Kamati, Augustino Vuma, amepongeza juhudi za benki hiyo katika kuboresha utendaji wake ndani ya kipindi kifupi.
“TCB imefanya mabadiliko makubwa sana. Tumeshuhudia ongezeko la mapato na utendaji mzuri katika kila eneo. Ninatoa pongezi kwa Bodi, Mtendaji Mkuu, na Menejimenti kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya,” amesema Vuma.
Aliongeza kuwa TCB imefanikiwa kutengeneza faida kubwa na inaendelea kukua kwa kasi. “Kwa sasa wanatarajia kutengeneza faida ya Shilingi bilioni 65 katika mwaka wa fedha ujao. Hii ni ishara ya fikra kubwa na uwekezaji wa kimkakati ambao hatukuwa tumezoea kuuona katika taasisi za umma,” amebainisha.
Vuma ameelezea kuridhishwa na ushirikiano wa TCB katika miradi ya kimkakati kama ununuzi wa mabehewa kwa ajili ya Shirika la Reli Tanzania (TRC). “Hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Ni jukumu la TCB kuhakikisha mipango iliyowekwa inatekelezwa kwa ukamilifu ili kuchochea tija na maendeleo,” amesema.
Amesisitiza kuwa gawio linalotolewa na TCB lina mchango mkubwa katika kuboresha huduma za kijamii nchini. “Fedha hizo zinaenda kugharamia miradi kama maji, umeme, na huduma nyingine muhimu katika maeneo mbalimbali ya nchi, mfano Igunga, Nkasi, Kilimanjaro, na Kasulu,” ameleza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Adam Mihayo, amesema ziara hiyo iliwapa fursa ya kueleza historia na mwelekeo wa benki hiyo kwa Kamati ya Bunge.
“Tumeshirikisha Kamati kuhusu safari yetu ya kutoka tulikotoka, tulipo sasa, na tunakoelekea. Tumepata maoni na maelekezo kutoka kwa Kamati ambayo tutayafanyia kazi,” amesema Mihayo.
Ameongeza kuwa serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wizara ya Fedha, ilitoa mtaji wa Shilingi bilioni 131 mwaka jana, ambao umekuwa chachu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano wa benki hiyo.
“Matokeo ya utekelezaji wa mpango huo yamekuwa mazuri. Hadi Septemba mwaka huu, tumetengeneza faida ya Shilingi bilioni 35 kabla ya kodi. Hii ni ishara kuwa tuko kwenye mwelekeo sahihi,” amesema Mihayo.
Aidha, ameishukuru serikali, Benki Kuu, na Kamati ya Kudumu ya Bunge kwa ushirikiano na miongozo inayotolewa, akibainisha kuwa hiyo imekuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya TCB.