Sheikh Hashim Ramadhani (wa nne kutoka kushoto), akitoa ufafanuzi wa huduma ya maji katika Quran, leo kabla ya mradi wa maji kukabidhiwa katika Gereza Kuu la Butimba, Mwanza.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation,Dkt.Alhaji Sibtain Meghjee, akitoa taarifa ya mradi wa maji katika Gereza Kuu la Butimba, leo.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, Masudi Kimolo (kulia),akipokea nyaraka za makabidhiano ya mradi wa kisima cha maji kutoka kwa Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Dkt.Alhaji Sibtain Meghjee (kushoto), leo.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Dkt.Alhaji Sibtain Meghjee (kushoto), leo akimkabidhi Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, Masudi Kimolo, majora ya vitambaa vya sare za wafungwa wa vifungo vya maisha.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Dkt.Alhaji Sibtain Meghjee (kushoto), Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, Masudi Kimolo (kulia), leo wakifungua koki za mabomba ya maji kundua mradi wa maji katika Gereza la Butimba.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, Masudi Kimolo (kulia),leo akizungumza na waandishi wa habari (haapo pichani)baada ya kukabidhia mradi wa kisima cha maji kutoka Taasisi ya The Desk & Cair Foundation.
Masheikh, Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation pamoja na maofisa wa Gereza Kuu la Butimba, leo wakishiriki kuomba dua baada ya kukabidhiwa mradi wa kisima na vifaa vya elimu.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation , Mkuu a Magereza Mkoa wa Mwanza Masudi Kimolo,leo wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa gereza hilo baada ya kukabidhiwa mradi wa kisima cha maji.Picha Zote na Baltazar Mashaka.
……..
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
TAASISI ya The Desk & Chair Foundation imekuwa mkombozi mkubwa katika kukabiliana na changamoto ya maji katika Gereza Kuu la Butimba, baada ya kutekeleza mradi mkubwa wa uchimbaji kisima kirefu.
Mradi huu wa kihistoria uliogharimu shilingi milioni 40, umelenga kutoa suluhu ya maji kwa zaidi ya watu 3,000 kila siku, wakiwemo maofisa wa gereza, askari, wafungwa, mahabusu na familia zao.
Katika hafla ya kukabidhi mradi huo leo, Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Dkt. Sibtain Meghjee, amesisitiza kuwa utapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya ukosefu wa maji na kuboresha afya za watumiaji wa maji gerezani.
“Mradi huu utahakikisha usafi wa mazingira,kupunguza magonjwa ya ngozi na kuhara, kuboresha afya ya wafungwa,mahabusu,askari na familia zao,” amesema Dkt.Meghjee.
Kwa mujibu wa Dkt. Meghjee, kisima hicho kirefu cha mita 100 kinatoa maji safi na salama, na mfumo wa usambazaji maji umejengwa kwa umakini mkubwa kuanzia nje hadi ndani ya gereza ambapo mradi huo umehusisha uchimbaji wa kisima kirefu, usimikaji wa pampu ya kusukuma maji, na ufungaji wa matangi matatu yenye uwezo wa kuhifadhi lita 1,000 kila moja.
Aidha, mradi huo umejumuisha ukarabati wa tanki la lita 15,000, kuunganishwa kwa maji kwenye ofisi za gereza, na uwekaji wa mifumo ya umeme kwa ajili ya pampu,pamoja na malipo ya Shilingi 550,000 za umeme wa luku.
Mbali na mradi wa maji, The Desk & Chair Foundation pia imesaidia vifaa vya elimu katika Gereza la Butimba, baada ya ombi la Kitengo cha Elimu ya Watu Wazima Jiji la Mwanza,ambavyo ni mbao za kufundishia, karatasi, kalamu, penseli, na majora mawili ya kushona sare za wafungwa.
Dkt. Meghjee amesema msaada huo ni juhudi za kuboresha elimu kwa wafungwa na mahabusu, ili kuwawezesha kupata ujuzi unaoweza kuwasaidia baada ya kumaliza kutumikia adhabu zao.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, Masudi Kimolo, ameeleza kuwa mradi huo wa maji utaondoa kero kubwa ya ukosefu wa maji, ambayo ilikuwa ni changamoto kubwa katika gereza hilo.
“Maji haya yatatumika kwa matumizi ya wafungwa, mahabusu, na familia za maofisa na askari. Pia, usafi wa mazingira na afya zao utaboreshwa. Pamoja na hayo, deni la shilingi milioni 400 linalotukabili katika gereza letu baada ya kupata mradi huu halitaongezeka,” amesema Kimolo.
Ameongeza kuwa miundombinu ya mradi huo itatunzwa kwa umakini ili kuhakikisha inakuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo mbapo ameahidi kuchukua hatua kali kwa watakaothubutu kuharibu au kuzuia utendelevu wa mradi huo kuwa, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahalifu wa aina hiyo.
Katika hatua nyingine, Kimolo ameishukuru The Desk & Chair Foundation kwa msaada mkubwa walioutoa, akisema utaendelea kuwa na manufaa makubwa si tu kwa wafungwa, bali pia kwa askari na familia zao.
“Tunawashukuru sana kwa msaada wenu, na tunatarajia msaada zaidi katika maeneo mengine ya maendeleo.Kwa ujumla, mradi huu unaonesha juhudi za The Desk & Chair Foundation katika kushughulikia changamoto za kijamii na kuboresha maisha ya watu, huku ukitilia mkazo katika afya, elimu, na usafi wa mazingira”,amesema.
Kimolo amesema mmsaada huo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi binafsi, serikali, na jamii katika kutatua changamoto zinazowakumba watu wengi.
Awali Sheikh Hashimu Ramadhan, alikumbusha kuwa mradi huo wa maji unalenga kutoa msaada kwa watu waliopo gerezani, na kwamba kutoa maji ni tendo la thawabu kubwa ka mujibu wa Quran.
“Maji ni muhimu katika uhai wa kila kiumbe, na kutoa maji kwa watu ni sadaka endelevu na thawabu maradufu.”amesena Sheikh Ramadhan huku akitaja kuwa gereza ni mahali pa kujifunza, kama ilivyo katika Qur’an, na kwamba wafungwa wanastahili kupata huduma muhimu kama maji, ili waweze kuishi kwa afya bora na ustawi.
Pai mradi huo wa The Desk & Chair Foundation ni mfano mzuri wa jinsi taasisi za kiraia zinavyoweza kushirikiana na serikali na jamii katika kutatua changamoto muhimu za kijamii.