Na Farida Mangube, Morogoro
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imetoa takribani shilingi bilioni 41 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya saba katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Ufadhili huu unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa elimu nchini.
Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 39.5 zitatumika kwa gharama za wakandarasi, huku shilingi bilioni 1.4 zikigharimia washauri waelekezi. Katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe, chuo hicho kitajenga majengo matano yatakayogharimu shilingi bilioni 19.2. Majengo haya yatakuwa na jengo la taaluma lenye uwezo wa kuchukua watu 3,500 kwa wakati mmoja.
Majengo mengine ni pamoja na jengo la taaluma la Ndaki ya Uchumi na Stadi za Biashara litakalojumuisha ofisi za watumishi, vyumba vya semina, na kumbi za mikutano zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja. Pia, kutakuwa na maabara ya bioteknolojia, maabara jumuishi, na maabara ya sayansi ya mimea.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi kati ya SUA na wakandarasi, iliyofanyika Kampasi Kuu ya Edward Moringe, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, alisema kuwa mradi huu unalenga kuboresha mitaala ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuongeza ubora wa usimamizi wa elimu ya juu nchini, hivyo kuchochea mchango wa vyuo vikuu kwenye uchumi wa taifa.
Katika Kampasi ya Solomon Mahlangu, chuo kitajenga majengo mawili yenye thamani ya shilingi bilioni 17.1. Majengo hayo ni jengo la taaluma lenye uwezo wa kuchukua watu 3,500 kwa wakati mmoja na hosteli yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 500.
Mhandisi Hanington Kagiraki, Mratibu wa Mradi wa HEET kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, alitoa wito kwa SUA kusimamia vyema ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
“Tunatarajia tupokee majengo yakiwa yamekamilika, yakiwa na vifaa vyote muhimu kama vitanda katika hosteli na viti na meza kwenye madarasa. Hatupendi kupokea majengo yasiyo na vifaa, kwani bila hivyo, inakuwa vigumu kutofautisha hosteli na madarasa,” alisema Mhandisi Kagiraki.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, alisema kuwa serikali ya mkoa itahakikisha ushirikiano na SUA ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Mradi huu unatarajiwa kuwa na majengo tisa yenye vyumba vya madarasa, hosteli za wanafunzi, maabara, karakana za uhandisi, pamoja na ofisi za watumishi. Utekelezaji wa mradi huu unalenga kuimarisha mazingira ya kujifunzia katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe na Kampasi ya Solomon Mahlangu zilizopo Morogoro, pamoja na Kampasi ya Mizengo Pinda iliyoko Katavi.