Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Serikali kupitia Mradi wa Uboreshaji Elimu ya Sekondari (SEQUIP) inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 1.16 katika mwaka wa fedha 2024/25 kujenga shule mpya mbili za sekondari wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Shule hizo zitajengwa katika maeneo mawili tofauti. Moja itajengwa katika Jimbo la Same Magharibi, Kata ya Hedaru (Shule mpya ya Hedaru – Mpatwa), na nyingine itajengwa katika Jimbo la Same Mashariki, Kata ya Kihurio (Shule ya Sekondari ya Ufundi). Kila jimbo litapokea zaidi ya shilingi milioni 584 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Akiwa katika Kata ya Hedaru kukagua ujenzi wa shule hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, alisema utekelezaji wa miradi hiyo upo katika hatua mbalimbali. Alisisitiza kwa wasimamizi kuhakikisha kwamba thamani ya fedha inaendana na ubora wa miradi, ili ziweze kuwa na matumizi endelevu. Aliongeza kuwa ifikapo tarehe 31 Desemba 2024, miradi yote inapaswa kukamilika.
“Muhimu ni kuhakikisha wahandisi wanamfuatilia mkandarasi kwa karibu ili kuepusha uzembe na hasara yoyote inayoweza kujitokeza,” alisema DC Kasilda
Aidha, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu ya elimu, akisema kuwa mradi huu unalenga kuondoa msongamano wa wanafunzi katika shule ya Sekondari ya Mkombozi, ambayo inahudumia wakazi wa Kata ya Hedaru.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkombozi na msimamizi wa ujenzi wa shule hiyo, Mwalimu Bakari Nyambwiro, alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa (majengo manne), ofisi mbili za walimu, jengo la utawala, maktaba, maabara nne (Fizikia, Baiolojia, TEHAMA na Kemia), matundu nane ya vyoo (4 kwa wasichana na 4 kwa wavulana), kichomea taka, na tanki la kuhifadhia maji.
Naye Diwani wa Kata ya Hedaru, John Kindori, alisema kuwa shule hii ni hitaji kubwa kwa wakazi wa eneo hilo, na itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani katika shule ya Sekondari ya Mkombozi. Walimu wa shule hiyo pia wamesema kuwa mradi huo utachochea ufaulu kwa wanafunzi.