Na Mussa John
Waandishi wa habari 36 kutoka mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Kagera, na Geita wamekutana mkoani Mwanza kwa mafunzo yaliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha waandishi hao kupata uelewa zaidi kuhusu majukumu ya Benki Kuu na hivyo kuandika kwa umahiri na usahihi zaidi katika masuala yanayohusu taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania tawi la Mwanza, Bi. Gloria Mwaikambo, alisema kwamba kwa zaidi ya miaka 12, imekuwa desturi ya BOT kukutana na waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo. Alieleza kuwa ushirikiano huu kati ya Benki Kuu na waandishi wa habari ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa taifa kwa ujumla.
“Benki Kuu inatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari, na kwa kutaja vyombo vya habari, ninamaanisha ninyi waandishi wa habari. Tunawashukuru kwa kuwa daraja muhimu linalotuwezesha kuwafikia wananchi kupitia habari na makala,” alisema Bi. Gloria Mwaikambo.
Kwa upande wake, Edwin Soko, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, akizungumza kwa niaba ya waandishi walioshiriki mafunzo hayo, ameishukuru Benki Kuu kwa kutambua umuhimu wa kuwajengea uwezo waandishi wa habari na kuendelea kushirikiana nao kwa manufaa ya jamii.