Na WAF, Dodoma
Serikali imetoa wito kwa Wizara, Idara na Taasisi nyingine kuongeza nguvu kwenye mapambano ya vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ili kufikia malengo ya kuzuia na kudhibiti magonjwa hayo.
Rai hiyo imetolewa Novemba 13, 2024 na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim James Yonazi katika ufunguzi wa kikao kazi cha Wakurugenzi, Rasilimali Watu na Wakurugenzi wa Sera kujadili mikakati ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza mahala pa kazi.
“Inatupasa kwa pamoja tuunganishe nguvu zetu kuzuia vihatarishi ambavyo ni kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na pombe, kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi na kujiepusha na tabia bwete, kuzingatia mlo unaofaa na kanuni bora za lishe,” amesisitiza Brigedia Jenerali Ndagala.
Brigedia Jenerali Ndagala amesema ipo haja ya kujipanga kukabiliana na madhara mengine yatokanayo na uharibifu wa mazingira na tabia nchi na kupitia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Muda ni sasa, zuia magonjwa yasiombukiza mahali pa kazi.
Brigedia Jenerali Ndagala amesema, lengo kuu la kaulimbiu hiyo ni kuitaka jamii ya Watanzania wakiwemo wafanyakazi na wadau wote kushirikiana kubadili mtindo wa maisha ili kuwa na afya bora na yenye kuleta tija kwa taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea amesema magonjwa yasiyoambukiza ni suala mtambuka ambalo linahusisha sekta zaidi ya moja zikiwemo wizara 15 zilizoshiriki kikao kazi hicho ili kufikia malengo ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.
“Kutokana na hali ya magonjwa yasiyoambukiza kuongezeka nchini, tunahitaji mpango kazi wa kitaifa na mfumo mzima wa Serikali ili kuisaidia jamii kwenye mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Dkt. Nyembea na kuongeza
“Huko nyuma ulaji wa ubwambwa ulikuwa mara moja kwa wiki, lakini hivi sasa hata mara tatu kwa siku mtu anakula, nyama zamani mtu anakula finyango mbili lakini sasa anakunywa supu ya nyama hata kilo nzima kwa siku,” amefafanua Dkt. Nyembea.