*Yapania kuchukua kombe msimu wa 2024
Na Mwandishi wetu, Tanga
Timu ya wanaume ya wavuta kamba ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) leo Novemba 13, 2024 imeshinda mechi ya mchezo wa kuvuta kamba dhidi ya PSSSF Kwa mivuto miwili bila majibu (2 – 0) katika Mashindano ya Mashirika ya Umma, Makampuni na Taasisi Binafsi (SHIMMUTA) yanayoendelea Mkoani Tanga.
Akizungumza Kwa niaba ya wachezaji wa timu ya mchezo wa Kamba ya TAWA Nahodha wa timu hiyo Jumanne Athumani ameishukuru Menejimenti ya taasisi hiyo Kwa kuwawezesha kushiriki mashindano hayo ambayo pamoja na mambo mengine amesema wanayatumia kuhamasisha utalii wa ndani Kwa vivutuo vya utalii vilivyopo TAWA.
Jumanne pia ameushukuru uongozi na walimu wa timu ya kamba Kwa kuendelea kuwapa mbinu mbalimbali za kuwakabili timu shindani katika mashindano hayo.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi wa TAWA Taifa Liwewa amesema ushindi walioupata dhidi ya PSSSF umekuwa chachu ya kuzidi kusonga mbele na kusisitiza kuwa malengo ya TAWA katika mashindano hayo ni kufika fainali na kuchukua ubingwa.
TAWA inashiriki mashindano hayo yaliyoanza Novemba 10, 2024 Jijini Tanga katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa Pete na mchezo wa kuvuta kamba ambapo inatajwa kufanya vyema katika michezo hiyo na kuonekana tishio kila iingiapo dimbani.
Ushiriki wa TAWA kwenye mashindano hayo sio tu unaleta ushindani Kwa timu pinzani, bali pia unajenga mshikamano wa ndani na kuimarisha afya za wahifadhi.