Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gelard Kusaya, amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi mkoani humo kuhakikisha wanasaidia serikali kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao, kufuatia fedha nyingi zilizotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya idara mbalimbali.
Kusaya alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) wilayani Serengeti, mkoani Mara. Alisema kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa viongozi katika ngazi husika, hususan watumishi wenye dhamana, kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
“Fedha zimepelekwa kila kona, na kila mmoja ana wajibu wa kuzisimamia; haiwezekani kazi hiyo aachiwe Rais peke yake,” alisema Kusaya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TALGWU mkoa wa Mara, Dk. Magreth Shaku, alisema kuwa viongozi pamoja na watendaji wengine wana wajibu wa kuisaidia serikali katika usimamizi wa shughuli za maendeleo na kudhibiti ubadhirifu katika maeneo yao.