Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Christian Nyakizee akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 8, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu
Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano na Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Christian Nyakizee.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufatilia miradi sita yenye thamani ya Shilingi 15,982,221,355.9 ambayo inaendelea na utekelezaji pamoja na kuwajengea uwezo Maafisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni pamoja na Askari Polisi Dawati la Jinsia na Watoto kwa ajili ya kutatua kero za ukatili wa kingono kwa watoto na jamii .
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 8, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia Julai 2024 hadi Septemba 2024, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Bw. Christian Nyakizee, amesema kuwa katika kufatilia miradi wamebaini mapungufu machache ambayo wahusika wameshauriwa kurekebisha, huku akisisitiza kuwa wanaendelea kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.
Bw. Nyakizee amesema kuwa katika kipindi hicho wametoa mafunzo kwa Maafisa Ustawi wa Jahmii kutoka kata zote za Manispaa ya Kinondoni ambapo washiriki walisisitiza umuhimu wa kutimiza wajibu wao kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo ili kuleta tija katika utendaji kazi na kufikia malengo.
“Pia Askari Polisi Dawati la Jinsia na Watoto walishiriki mafunzo ili kushughulikia kero za Dawati kwa ufanisi ikiwemo vitendo vya rushwa na kurahisisha utendaji kazi wa Dawati ” amesema Bw. Nyakizee.
Amefafanua kuwa jumla ya Askari Polisi 37 kutoka kwenye madawati 14 ya Manispaa ya Kinondoni waliofanikiwa kushiriki mafanzo ikiwemo Oysterbay, Kijitonyama, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Magomeni, Urafiki, Mburahati, Gogoni, Magufuli Bus Terminal, Mavurunza, Kawe, Mbweni, Mabwepande, Goba pamoja na Madale.
Ameeleza kuwa pia wamepokea jumla ya malalamiko 104, huku Malalamiko yaliyohusu rushwa yakiwa 72 na yasiyohusu rushwa ni 32.
Bw. Nyakizee amesema kuwa wamefungua mashauri mapya mawili, katika Mahakama ya Wilaya ya Ubungo, Mashauri saba yalitolewa maamuzi, na Jamhuri imeshinda mashauri matatu, Mashauri 24 yanaendelea Mahakamani
“Tumejipanga vizuri kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuelimisha Wananchi wajue madhara ya rushwa na wahamasike kushirikiana na TAKUKURU kutokomeza rushwa” amesema
Bw. Nyakizee.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelee kutoa ushirikiano na kuwasihi kuendelea kutoa taarifa za rushwa kwa kupiga au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa kutumia namba ya dharura 113 na kufuata maelekezo au kufika katika ofisi yoyote ya TAKUKURU.