Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya Elimu Duniani (GPE)katika picha ya pamoja na Mhe. Ahmed Hussein, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada (kushoto) na Bw. Charles North, Naibu Mtendaji Mkuu wa GPE.
…………………
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya Elimu Duniani (GPE) ameongoza ujumbe wa Taasisi hiyo ya GPE kukutana na kufanya mazungumzo leo na Mhe. Ahmed Hussein, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, jijini Toronto, Canada.
Rais Mstaafu Dkt. Kikwete aliyeambatana na Bw. Charles North, Naibu Mtendaji Mkuu wa GPE, ametumia fursa ya mkutano huo kuishukuru Serikali ya Canada kwa kuendelea kufadhili miradi ya elimu katika nchi 90 zinazoendelea zinazohudumiwa na Shirika la GPE, ikiwemo Tanzania.
Aidha, Viongozi hao wameongelea namna Canada na GPE zinavyoweza kukuza ushirikiano huo, hususan kwa kipindi ambacho Canada inaenda kuchukua Urais wa Kundi la Mataifa yaliyostawi zaidi Kiuchumi (G7) mwaka 2025.
Rais Mstaafu yupo Canada kuhudhuria Mkutano kati ya Canada na Umoja wa Afrika (AU) akiwakilisha Taasisi za GPE pamoja na Shirika la Kimataifa la Lishe la Canada (Nutritional International, NI) ambapo yeye ni Mjumbe wa Bodi.
Akiwa nchini Canada, Rais Mstaafu anatarajiwa pia kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Canada yanayolenga kukuza mahusiano kati ya Canada na Taasisi ya GPE na Shirika la NI.