Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla akizungumza na Wanachama pamoja na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Temeke katika Ukumbi wa TPA SABASABA, leo NOV 08, 2024.
………
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, ametoa msisitizo kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutenda haki kwa vyama vyote vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Amesema katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, wapo wagombea wa CCM ambao wamewekewa pingamizi, hivyo madai ya vyama vya upinzani kwamba wagombea wao pekee ndiyo waliowekewa pingamizi yanalengo la kuwahadaa Watanzania.
CPA Makalla aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam leo, ambapo alisisitiza CCM ipo tayari kushiriki uchaguzi huo na kitaibuka mshindi kwani kimejiandaa ipasavyo.
“Nitume nafasi hii kuwaomba TAMISEMI ambao ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huu, waitendee haki CCM na vyama vingine vyote vitendewe haki. Tunaamini uchaguzi utakuwa huru na haki na atakayeshinda kwa haki, atangazwe.
“CCM hatuhitaji upendeleo, hatuhitaji kubebwa, tuko tayari kwani tulishajipanga. Hatuhitaji mbelekeo na TAMISEMI itende haki kwa vyama vyote vya sisasa vilivyoweka wagombe na sisi tupo tayari kushindana na tutashinda kwa haki,” alisisitiza.
Alieleza kuwa hata wagombea wa CCM wapo waliowekewa mapingamizi, lakini vyama vya upinzani vinataka kuwadanganya Watanzania kama vile wagombea wao tu ndiyo wamewekewa mapingamizi.
“Wagombea wa CCM wamewekewa mapingamizi katika baadhi ya maeneo kama vile baadhi ya vyama vingine walivyowekewa mapingamizi. Haiwezekani wakati wagombea wa CCM wamewekewa mapingamizi alafu waonyeshe wao tu kwamba wamewekewa mapingamizi.
“Juzi nilisema Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu ametamka bayana kwamba CHADEMA hawana uwezo wa kuweka wagombea kila maeneo. Baada ya kusema hivyo sasa wamejipanga kumrushia madongo.
Aliongeza kuwa: “Mlisikia jana walisema katika Mkoa wa Dar es Salama wameweka wagombea 540 ni waongo, yote ni kumpiga Tundu Lissu na leo najua Mnyika ataongea anataka kutoa takwimu za kusimamisha wagombea za kuwahadaa Watanzania kwamba wamejipanga lakini kumbe ni uongo.”
Makalla alisema chama hicho kimepoteza muda mwingi katika maandamano, hivyo katika uchaguzi huu hawajajipanga kwani kina mgogoro mingi ndani.
“Katika chama chao kuna CHADEMA Lissu na CHADEMA Mbowe, wanavutana na ndiyo maana mnawaona hawaongei, hawapo tayari kwenye uchaguzi huu na CCM tutumia nafasi hii kushinda uchaguzi huu.
“Hakuna demokrasia iliyoporwa, Rais Dk Samia kupitia 4R ndiye aliyewaruhusu wafanye mkutano. Ndiye aliyewaruhusu wafanye ziara. Hakuna demokrasia iliyoporwa, wanatafuta sababu za kuthibitisha kushindwa kwao mapema. Wanataka kuwahadaa Watanzania kama vile wanaonewa kumbe ni waongo. chama chao kimepoteza dira na mwelekeo wasitafute kisingizio,” alisisitiza CPA Makalla.