Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude akizungumza katika leo, Novemba 7, 2024, katika kikao kazi cha wahariri wanaoripoti habari za Wizara ya Fedha kilichofanyika mjini Morogoro.
Benny Mwaipaja Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wizara ya Fedha akizungumza katika kikao kazi kati ya wahariri na wizara hiyo mkoani Morogoro Leo Novemba 07, 2024.
………….
NA JOHN BUKUKU, MOROGORO
Serikali ya Tanzania imeripoti kuwa Pato la Taifa limeongezeka kwa asilimia 5.4 mwaka 2024, huku viashiria vya uchumi vikiendelea kuimarika kutokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji, na huduma za kijamii.
Akizungumza leo, Novemba 7, 2024, katika kikao kazi cha wahariri wanaoripoti habari za Wizara ya Fedha kilichofanyika mjini Morogoro, Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, alisema ukuaji wa Pato la Taifa umechangiwa zaidi na sekta za ujenzi, kilimo, na uchimbaji wa madini.
CPA Mkude aliongeza kuwa, Pato la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 5.8 mwaka 2025, akibainisha kuwa ukuaji huo utatokana na miradi ya kimkakati katika sekta ya nishati na usafirishaji pamoja na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi.
“Pia, jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, pamoja na utawala bora na huduma za kijamii, zimechangia kwa kiasi kikubwa,” alisema CPA Mkude.
Aidha, CPA Mkude alibainisha kuwa shughuli za kiuchumi zinaendelea kuimarika nchini licha ya changamoto za migogoro ya kikanda na kimataifa pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Katika hatua nyingine, alieleza kuwa Serikali imefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei kutokana na sera thabiti za Wizara ya Fedha, ambapo inatarajiwa kuwa mfumuko wa bei utakuwa chini ya lengo kwa asilimia 3 hadi 5.
Vilevile, CPA Leonard Mkude alitangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano mkubwa wa wahasibu na wakaguzi wa hesabu kutoka nchi zaidi ya 30 za Afrika, utakaofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa AICC jijini Arusha kuanzia Desemba 3-5, 2024.
Mkutano huo unalenga kuwakutanisha wataalamu wa masuala ya fedha na ukaguzi ili kujadili changamoto na fursa zilizopo kwenye sekta hiyo barani Afrika. Pia, utatoa jukwaa la kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusu mbinu za kisasa za usimamizi wa fedha na ukaguzi, ili kuchangia katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwenye sekta ya umma na binafsi.
Rais Samia anatarajiwa kutoa hotuba ya ufunguzi, akisisitiza umuhimu wa uadilifu na uwazi katika usimamizi wa fedha kama njia ya kuchochea maendeleo na kuimarisha uchumi wa nchi za Afrika.
Washiriki wa mkutano huo pia watapata fursa ya kutembelea vivutio vya utalii mkoani Arusha, kama Mbuga za Wanyama za Serengeti, Ngorongoro Crater, na Arusha National Park, miongoni mwa vingine vingi.
Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika sekta ya utalii wa mikutano, ikivutia mikutano mingi ya kimataifa kutokana na amani na utulivu uliopo nchini. Pia, jitihada za Rais Samia za kuifungua nchi kiuchumi na kuvutia watalii kupitia filamu ya Royal Tour zimechangia kuwavutia watalii wengi kuja kutembelea vivutio vya Tanzania.