Havana, 07 Novemba, 2024
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuutaarifu umma kwamba ziara ya kitaifa ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopangwa kufanyika tarehe 6 hadi 8 Novemba, 2024 nchini Cuba imeahirishwa.
Ziara hiyo imeahirishwa kufuatia taarifa rasmi iliyowasilishwa na Serikali ya Cuba ikitaarifu kutokea kwa mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yangehatarisha usalama wa watu na mali zao.
Aidha, taarifa hiyo ilibainisha kuwa nchi ya Cuba itakumbwa na kimbunga Rafael kuanzia tarehe 6 hadi 7 Novemba, 2024. Hali hiyo imepelekea Serikali ya Cuba kuchukua tahadhari ikiwemo kusitisha safari zote za ndege kuingia na kuondoka Cuba.
Pamoja na kuahirishwa kwa ziara hiyo, Mhe. Rais ameelekeza shughuli zote zilizopangwa kufanyika kipindi cha ziara yake ziendelee kuratibiwa chini ya Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akishirikiana na Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Ziara nyingine ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Cuba itapangwa siku za usoni baada ya nchi hizo mbili kukubaliana wakati sahihi wa ziara hiyo
Dar es Salaam, 6 Novemba, 2024
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali