Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media Same Kilimanjaro
WANANCHI wa Kata ya Kihurio wilayani Same Mkoani Kilimanjaro wameishukuru Serikali kuwapatia mradi mkubwa wa maji unaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 4.17 ambao utakuwa mwarobaini wa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi zaidi ya 10,000 wa Kata hiyo.
Pili Salim, ni miongoni mwao Wakazi wa Kata hiyo ambaye alisema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa suluhisho juu ya adha wanayoipata ya kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji kwenye mito.
Kauli ya Wananchi hawa inaungwa mkono na Katibu wa Mbunge Jimbo la Same Mashariki, Semu Mmamba ambaye alisema huduma ya maji ni hitajio kubwa kwa Wananchi wa Kihurio, akiomba mkandarasi kuanza utekelezaji wa mradi huo kama mkataba unavyomtaka.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Meneja wa Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Abdallah Gendaeka amesema, mradi utatekelezwa kwa muda wa miaka miwili kuanzia Desemba 06 mwaka huu na kutarajiwa kukamilika Desemba 06 mwaka 2026.
Alisema kuwa kazi hiyo itafanywa na mkandarasi kutoka kampuni ya FESAM CONSTRUCTION LIMITED yenye makao makuu yake Jijini Dar es Salaam (mkandarasi mzawa).
Kwa upande wake, Meneja wa Ruwasa mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Weransari Munisi, alisema kuwa kupaatika kwa fedha za mradi huo kunachagizwa na jitihada za Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Anne Kilango kwa lengo la kutaka Wananchi wake kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.