Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) Nd. Mtumwa Said Sandal akizungumza na Watumiaji wa Bandari ya Funguni Malindi Zanzibar na Wafanyakazi wa Ofisi ndogo ya ZMA Mkokotoni wakati alipofanya ziara ya kikazi kusikiliza changamoto zao.
……..
Takdir Ali. Maelezo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) Nd. Mtumwa Said Sandal amewataka Wafanyakazi kushirikiana na kuwa wazalendo wa kutekeleza majukumu yao ili waweze kuleta ufanisi katika kazi.
Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati alipofanya ziara ya kikazi kwa ajili ya kusikiliza changamoto za Watumiaji wa Bandari ya Funguni Malindi Zanzibar na Wafanyakazi wa Ofisi ndogo ya ZMA iliyopo Mkokotoni.
Amesema mashirikiano ya pamoja yanapelekea kuwajibika ipasavyo na kufikia malengo waliojipangia ya kusimamia usalama wa vyombo vya usafiri wa Baharini na kukuza Uchumi wa Nchi.
Aidha, Mkurugenzi huyo ameahidi kushirikiana na Mamlaka husika katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakabili watumiaji wa Bandari ya Funguni Malindi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Nao Watumiaji wa Bandari ya Funguni Malindi wamesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa Taa katika eneo hilo jambo ambalo linasababisha kufanyika kwa vitendo vya Wizi wa vitendea kazi vyao hasa Mashine za vyombo vya usafiri.
Hivyo waiomba Mamlaka kusaidia upatikanaji wa huduma ya uwekaji wa Taa katika eneo hilo ili kupunguza vitendo vya wizi.
Kwa upande wake Mkuu wa ZMA Ofisi ndogo Mkokotoni Simai Nyange Simai amesema ziara ya Mkurugenzi huyo imewapa moyo na kuongeza motisha katika usimamizi na utendaji wa Kazi zao za kila siku.
Aidha amewaomba Wafanyakazi wenzake kujitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kusimamia utekelezaji wa mpango kazi wa Mamlaka hiyo kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.
Nao Wafanyakazi wa ZMA Ofisi ndogo Mkokotoni wameomba kufanyiwa ukarabati wa Paa, Maji Safi na Salama, Vitendea kazi, Fotokopi na Printa ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Mbali na hayo wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka Mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kuahidi kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi yao na Taifa kwa Ujumla.