Na Mwandishi wetu, Mirerani
ELIKANA Sanaya (Nyundoo) ni meneja wa kampuni ya Iraq Mining LTD kupitia Mkurugenzi wake Emmanuel Joseph Wado (Sunda) inayochimba madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Ukimzungumzia meneja wa kampuni ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani anayewajali wachimbaji na wafanyakazi wa migodi yao huwezi kuacha kumtaja mtu bingwa kabisa Nyundoo.
Nyundoo akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Gracian Max Makota, ameishukuru Serikali na chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani kwa kutambua mchango wake kwa wachimbaji.
Ametoa wito kwa mameneja wote wa migodi ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani kuwajali na kuwapenda wafanyakazi wa migodi yao hata wakipata changamoto ya ugonjwa.
“Ukiwa na mfanyakazi kwenye mgodi wako kisha akaumwa unatakiwa kuhakikisha amepata matibabu na siyo kumtupa na kumjali wakati akiwa mzima tuu na mwenye nguvu za kufanya kazi,” amesema Nyundoo.
Amesema ukiwa kiongozi unapaswa kuwajali wafanyakazi wako na Mungu atakulipa kwani wanafanya kazi kwa moyo mmoja na hata ikitokea changamoto unapaswa kuwasaidia.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, MAREMA Tawi la Mirerani Rachel Njau amesema Nyundoo ni aina ya mameneja wachache wenye kuwajali wafanyakazi wao.
“Ukimpigia simu Nyundoo na kumueleza kuwa kuna mgonjwa wa mgodini kwao amefika ofisini akiwa na tatizo la maradhi au fedha zozote amekuwa mwepesi kwa kutoa hata fedha za mfukoni mwake kisha atawasiliana na mkurugenzi wake Sunda baadaye,” amesema Rachel.
Amesema kutokana na hali hiyo hivi sasa hakuna tena wachimbaji au wafanyakazi wa kampuni ya Iraq Mining LTD wanaofika kwenye ofisi hiyo na kulalamikia haki zao.
“Tunampongeza Mkurugenzi wa kampuni hiyo Emmanuel Joseph Wado na Meneja wake Nyundoo kwa kuwajali wachimbaji na wafanyakazi wao,” amesema Rachel.
Amewasihi baadhi ya wakurugenzi na mameneja wasiowajali wafanyakazi wap kubadilika na kuiga mfano wa meneja Nyundoo ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuwajali wachimbaji wake.
“Mnapokuwa na Meneja kama Nyundoo anayewajali wachimbaji na wafanyakazi wake kwenye sekta ya madini ya Tanzanite sisi viongozi wa wachimbaji tutakuwa tunafanya kazi kwa ufanisi na ushirikiano mkubwa,” amesema.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota, akimkabidhi Nyundoo cheti cha kutambua mchango wake kwa wachimbaji, amempongeza kwa namna anavyowajali wachimbaji wake.