Ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Ilala imepokea malalamiko themanini na mbili (82) ambapo uchambuzi umeonyesha yanayohusiana na rushwa ni 68 tu, hivyo wahusika wa taarifa 14 zisizohusiana na rushwa walishauriwa na kuelekezwa katika idara stahiki na taarifa zao zikafungwa.
Hayo yameelezwa na Bw. Sosthenes W. Kibwengo,Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Ilala jijini Dar es Salaam Leo Novemba 02, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za taasisi hiyo Upanga
Bw. Kibwengo amesema taarifa zilizohusu rushwa zilishughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 kama ilivyorejewa mwaka 2022 na ambazo zilihusu sekta na maeneo yafuatazo: Fedha (20); Binafsi na Serikali za mitaa (kila moja 9); Ardhi na Polisi (kila moja 7); Biashara, TRA na Mahakama (kila moja 3); na nyinginezo (7).
Aidha ameeleza kuwa majalada matatu ya uchunguzi yaliwasilishwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, na mashauri mapya sita (6) yamefunguliwa mahakamani yakihusisha washtakiwa 13 kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya ubadhirifu na utakatishaji fedha haramu wa jumla ya shilingi Bilioni nne, milioni mia nane tisini na moja laki tatu sabini na sita elfu mia tano sitini (4,891,376,560).
Ameeleza kuwa Mashauri 7 yamekamilika na Jamhuri imeshinda mashauri mengine 6, na mashauri 35 yanaendelea mahakamani.
Aidha waliotiwa hatiani wapo ambao wametakiwa pia kurejesha shilingi 51,500,000/= walizofuja na tayari shilingi 15,500,000/= zimeshalipwa.
Vilevile, amefafanua kuwa ufuatiliaji katika eneo la uchunguzi na uzuiaji rushwa kwa kushirikiana na wadau wengine umewezesha kuokoa/kudhibiti jumla ya shilingi 66,280,000/=.
Amesema TAKUKURU itaendelea na uelimishaji wa Tambua thamani ya kura ili kuwaandaa wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Aidha, watafanya semina ya viongozi wa dini ili kuwaomba watumie nyumba za ibada kuelimisha waamini na waumini wao kujiepusha na rushwa kwenye uchaguzi na kwa ujumla wake kwani rushwa ni dhambi.
Kibwengo ameongeza kuwa vilevile wataendelea kuweka nguvu katika kundi la vijana ambao ndio chachu ya mabadiliko chanya katika jamii kupitia klabu za wapinga rushwa na shindano la kuandaa na kutuma jumbe fupi na picha jongefu (video clips) zinazotoa elimu ya kujiepusha na rushwa katika uchaguzi na kuhamasisha jamii kuchagua viongozi waadilifu.
Amewakumbusha wananchi kwamba Kiongozi anayeingia madarakani kwa rushwa hawezi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa, hivyo tuchague viongozi waadilifu na wasiojihusisha na rushwa. Usinunulike kwani thamani ya kura yako ni maendeleo. RUSHWA HAILIPI.