Na: Dk. Reubeni Lumbagala.
Jana nilianza sehemu ya kwanza ya mada isemayo “CBE ilivyotumia ubia kuboresha elimu.”
Katika makala ile nilieleza umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP) katika kuchagiza maendeleo.
Nilieleza kwa ufupi namna ambavyo Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) kilivyoamua kushirikiana na sekta binafsi kutatua tatizo la uhaba wa mabweni Kwa kuunganisha nguvu ya pamoja kujenga mabweni.
Sasa endelea na sehemu ya pili:
Kwa mujibu wa Mkuu wa chuo cha CBE, Prof. Edda Lwoga, ubia huu unatokana na changamoto ya mabweni katika chuo cha CBE ambapo katika kampasi yake kuu jijini Dar es Salaam, chuo kina wanafunzi 12,000 lakini mabweni yaliyopo ni mawili tu yenye uwezo wa kuchukua vitanda 160 pekee vya wanafunzi wa kike na kiume. Vitanda hivi 160 ni sawa na aslimia 1.34 huku kukiwa na upungufu wa vitanda kwa asilimia 98.6.“Mradi huo utafanywa kwa ubia kati ya CBE na mwekezaji lakini pia naomba nitumie nafasi kuwafahamisha wadau, wawekezaji wa ndani na nje kuhusu fursa hii muhimu ya uwekezaji ili waweze kushiriki kwenye mkutano maalumu utakaokutanisha wadau mbalimbali katika kuupelekea mradi huu sokoni na kupeana uwelewa zaidi na mkutano huo utafanyika tarehe 20 siku ya ijumaa,” alisema Prof. Lwoga.
Ubia kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu kutokana na uwepo wa changamoto katika sekta ya elimu kama vile upungufu wa madarasa, madawati, meza, viti, mabweni, mabwalo, nyumba za walimu, kumbi za shule, mafunzo kazini kwa walimu na vifaa vya Tehama kutaja kwa uchache .
Nguvu ya pamoja baina ya sekta hizi mbili inachagiza utatuzi wa changamoto katika sekta ya elimu. Uwepo wa uhitaji mkubwa wa mabweni katika chuo cha CBE utapungua kwa kutoka asilimia 1.34 iliyopo sasa hadi asilimia 30 pindi mradi huu wa ujenzi wa mabweni utakapokamilika.“Hali iliyopo imesababisha uhitaji mkubwa wa malazi ya wanafunzi kwa asilimia 98.6 hivyo wengi wanalazimika kutafuta malazi nje ya chuo kwa gharama kubwa, jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu gharama hizo.
Njia ya PPP ni bora na ya haraka kufanikisha mradi huu, ambayo itawanufaisha wanafunzi na taasisi. CBE imejikita katika kutoa mazingira bora ya kujifunzia na uboreshaji malazi ya wanafunzi ni kipaumbele muhimu kwetu nawashukuru washirika wa sekta binafsi, serikali na wadau wote kwa mchango wao katika kufanikisha mradi huu muhimu,” anasema Prof. Lwoga.
Septemba 20, 2024, Kamishna wa PPP, David Kafulika alipongeza ubunifu uliofanywa na CBE katika kutatua changamoto ya mabweni, na hivyo kutoa wito kwa vyuo vingine kuihusisha sekta binafsi katika ujenzi wa mabweni na miradi mingine ya maendeleo. “Kila mradi ambao sekta binafsi inaweza kuutekeleza kwa teknolojia ya hali ya juu kuliko serikali basi apewe autekeleze ili tujenge uchumi wa kisasa ambao sekta binafsi ndiyo ina nafasi kubwa ya kutengeneza ajira nyingi.
Utaratibu wa ubia unaleta unafuu kwa serikali kwa sababu miradi inajengwa bila kutegemea fedha zake lakini utaratibu huu wa ubia unafanya serikali ivute teknolojia ya kujenga baadhi ya miradi, teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa inapatikana sekta binafsi,” amesema Kafulila.
Sekta binafsi ina nguvu ya raslimali fedha, ujuzi, uzoefu na teknolojia katika kumudu majukumu ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya elimu. Kwahiyo, ni muhimu kwa viongozi serikalini kuishirikisha ipasavyo sekta binafsi katika miradi mbalimbali ya elimu ili kuboresha sekta ya elimu.
Sanjari na hilo, ni muhimu kuzingatia kuwa ubia kati ya serikali na sekta binafsi si ubinafsishaji. Ubia ni kuunganisha nguvu ya pamoja, miradi ya ubia inabaki kuwa mali ya serikali, huku sekta binafsi ikiwa mshirika muhimu, na baada ya sekta binafsi kurejesha gharama zake za uwekezaji kwa mujibu wa mikataba, miradi hiyo huwa mali ya serikali kwa asilimia 100.Ni vyema sekta binafsi ikapewa ushirikiano badala ya kuwekewa vigingi katika kuboresha sekta ya elimu kwani ni wadau muhimu wa maendeleo.
Naamini miradi ya ubia katika sekta ya elimu ni muhimu sana kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu.
Mwandishi ni Mwalimu wa Sekondari ya Mlali ya mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.