Na Farida Morogoro
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, inaandaa mpango wa ushirikiano wa kubadilishana wataalamu na kufanya tafiti za pamoja kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Ushirikiano huu unatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania na kuimarisha maendeleo baina ya nchi hizo mbili.
Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakati wa ziara ya Waziri wa Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Bonginkosi “Blade” Nzimande, Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Prof. Ladislaus Mnyone, alisema kuwa mpango huu wa ushirikiano unalenga kupata wanafunzi na wataalamu kutoka Afrika Kusini kuja Tanzania ili kuimarisha uwezo wa kitaaluma na kiteknolojia.
Waziri wa Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Bonginkosi “Blade” Nzimande, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya nchi yake na SUA katika nyanja za utafiti, teknolojia, na programu za kubadilishana uzoefu kwa wanafunzi na wataalamu. Alisema kuwa hatua hii itachochea maendeleo katika sekta ya kilimo na kuleta manufaa kwa wananchi wa nchi zote mbili.
Aidha, Waziri Nzimande alibainisha kuwa ushirikiano wa kufanya tafiti kwa pamoja kati ya Tanzania na Afrika Kusini unaweza kuzaa matokeo yenye manufaa si tu kwa nchi hizi mbili, bali kwa bara zima la Afrika. Aliongeza kuwa Serikali ya Afrika Kusini itaangalia uwezekano wa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Afrika Kusini kuja kusoma katika vyuo vya Tanzania, ikiwemo SUA.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda, alisema SUA ina matarajio ya kupata wanafunzi kutoka Afrika Kusini, hasa ikiwa mtazamo hasi kuhusu elimu inayotolewa Tanzania utabadilishwa. Alieleza kuwa chuo hicho kimejipambanua kwa kutoa elimu bora na wataalamu mahiri katika nyanja mbalimbali barani Afrika.
Prof. Chibunda alihitimisha kwa kusema kuwa kama kutatolewa ufadhili kwa wanafunzi wa Afrika Kusini, wataleta mchango mkubwa kwa maendeleo ya sekta ya elimu na pengine kuamua kubaki Tanzania kutokana na mazingira ya amani na utulivu yaliyopo nchini.