Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali wakati wa Kikao cha nne, Mkutano wa 17 wa Bunge, bungeni jijini Dodoma leo Novemba mosi, 2024.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa Kikao cha nne, Mkutano wa 17 wa Bunge, bungeni jijini Dodoma leo Novemba mosi, 2024.
…………
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeandaa Mpango wa Kuirithisha Zanzibar ya Kijani ambao unalenga kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ameliarifu Bunge jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Azan Mwinyi lililoulizwa kwa niaba yake na
Mbunge wa Donge Mhe. Soud Mohammed Jumah kuhusu mkakati wa Serikali wa kunusuru vipando visivyohimili maji ya bahari katika Bonde la Tibirinzi Chakechake, Pemba.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Khamis amesema mpango huo unatarajiwa kusaidia katika upandaji na utunzaji wa miti hususan kwenye maeneo ya fukwe ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Naibu Waziri Khamis amesema SJMT kwa kushirikiana na SMZ imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ujenzi wa matuta ya kuzuia maji bahari yasiingie katika
mabonde ya kilimo ikiwemo Kisiwa Panza, Kilimani, Msuka, Sipwese, Micheweni na Tovuni.
Sanjari na hilo, amesema pia Serikali imechukua hatua ya kuwezesha upandaji wa miti ya aina mbalimbali ikiwemo mikoko au mikandaa katika maeneo ya fukwe ili kupunguza kasi ya uingiaji wa maji bahari katika maeneo hayo.
Mhe. Khamis ameongeza kuwa Serikali zote mbili zinaendelea kutafuta fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kuendelea kuweka miundombinu wezeshi inayozuia maji bahari kuingia katika makazi na maeneo ya kilimo
ikiwemo bonde la Tibirinzi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Khamis amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha ujenzi wa tuta moja kwa ajili ya kuzuia maji ya bahari yasiingie kwenye makazi ya wananchi katika eneo la Sipwese, Pemba
Amesema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Maryam aliyetaka kufahamu ni lini mradi huo utakamilika huku akifafanua kuwa ujenzi wa tuta lingine unatarajiwa kukamilika Desemba 2024.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri Khamis amesema kuwa dhamira ya Serikali zote mbili ni kutatua changamoto za mazingira zinazotokea hivyo zinaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga kuta katika ufukwe wa bahari
eneo la Nungwi.
Amesema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nungwi Mhe. Simai Hassan Sadiki aliyetaka kujua hatua iliyofikiwa na SJMT na SMZ katika ujenzi wa kuta eneo la Nungwi.