RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi Bilioni Nane kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mazoezi vitakavyotumika kwenye Mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027.
Hayo yamebainishwa Novemba 1, 2024 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa wakati akisaini Mkataba wa ujenzi na Suma JKT utakaojengwa siku 120.
“Tayari mchakato umeanza wa ukarabati wa viwanja kikiwamo cha Meja Jenerali Isamuhyo, Gymkhana, Shule ya Sheria ‘Law school’ na ujenzi wa viwanja vipya Leaders, Farasi, Tirdo na Gymkhana,”alisema Katibu Mkuu Msigwa.
Alisema kuwa ujenzi huo utahusisha uwekaji wa taa, majukwaa yatayochukua watu 2,000 katika viwanja vipya, njia za kupitisha maji na kupanda nyasi halisi Ili kuendana na viwango vya CAF. Akiongeza kuwa, mipango ni kujenga viwanja vitano vya mazoezi katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Arusha.
Ameongeza kuwa, sambamba na CHAN na AFCON, Serikali imekusudia kuwania kuwa wenyeji wa michuano ya All African Games ya mwaka 2027.
Naye Mkurugenzi wa uendeshaji wa Kampuni ya Suma JKT Morgan Nyonyi, alisema wapo tayari kufanya kazi usiku na mchana Ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
“Tayari kazi imeanza na leo tumesaini mkataba na tulianza na uwanja Meja Jenerali Isamuhyo na CAF walipita na kutupa baadhi ya maelekezo, na sasa tunaendelea na mchakato mzima wa uboreshaji na ujenzi wa viwanja vitano vya mazoezi,” alisema Bw. Nyoni.