Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha Uongozi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari amesema kuwa, TLS ni mdau muhimu katika kuishauri Serikali kwa kubaini mambo muhimu yaliyopo katika utekelezaji wa Sheria mbalimbali Nchini na hivyo ujio huo ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano baina ya pande hizo mbili.
Mwanasheria Mkuu ameyasema hayo Leo tarehe 1 Novemba, 2024 ofisini kwake Bungeni jijini Dodoma wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa TLS walipofika kwa ajili ya kujitambulisha, kufahamiana na kuboresha mahusiano baina ya Ofisi hizo.
“TLS ni mdau wetu mkubwa hivyo tunathamini sana ujio wenu na tunaamini itaongeza wigo wa ushirikiano katika utendaji kazi”Alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Rais wa TLS Wakili Boniphace Anyisile Kajunjumele Mwabukusi amesema TLS inaiona Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni nyumbani hivyo pande hizi mbili zinapaswa kushirikiana kwa maslahi ya Wanasheria na Taifa.
“Tunapenda TLS ifanye kazi kwa maadili Uwakili wetu uwe credible tunaweza kushindana na kuvutia watu wa au aina tofauti tofauti kwa kuzungumza na kuimarisha Sheria kwa manufaa ya Taifa letu.”Alisema Rais wa TLS
Kwa upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel Maneno amesema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sasa imepiga hatua kubwa katika matumizi ya mifumo mbalimbali ili kuimarisha na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na mfumo wa OAG-MIS unaowezesha upatikanaji wa Sheria mbalimbali pamoja na Sheria zote zilizofanyiwa Marekebisho.
Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu amemuomba Rais wa TLS kutumia majukwaa yao kutangaza mafanikio ya mfumo huo.