Katibu MKuu Wizara Maji Nishati na Madini Zanzibar Joseph John Kilangi azungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Maji Nishati na Madini Zanzibar na Wizara ya Nishati na Madini ya Jamuhuri ya Muungano waTanzania katika kikao cha wafanyazi killichofanyika katika ukumbi wa wizara hiyo Maisara Mjini Zanzibar
………
Na Imani Mtumwa. Maelezo
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar Joseph J. Kilangi amesema ni muhimu kuendeleza ushirikiano baina ya Wizara hiyo na Wizara ya Nishati na Madini ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania ili kuendelea kujadili mambo mbali mbali yanayohusu Wizara hizo.
Ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi kati ya Wafanyakazi wa Wizara ya Maji Nishati na Madini Zanzibar na Wizara ya Nishati na Madini ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukumbi wa Wizara hiyo Maisara amesema kuwepo kwa mashirikiano hayo itapelekea kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili katika majukumu ya kazi za kila siku.
Aidha amesema kufanyika kwa kikao hicho kutasaidia kupanga mikakati mbali mbali kwa kuangalia maeneo yanayoweza kuzalisha nishati ya umeme ili kuwa na umeme wa uhakika Nchini.
Akizungumzia kuhusu nishati safi ya kupikia amesema kadri vikao hivyo vitakapoendelea, watendaji watajadili jinsi ya upatikaji na usambazaji wa nishati hiyo ili iweze kukubalika kwa wananchi na kuwafikia kwa haraka watumiaji vijijini Unguja na Pemba.
“Maendeleo ya Nchi hayapatikani bila ya kuwepo nishati ya uhakika hivyo wizara zetu hizi zimekamata ileijini ya maendeleo ya Nchi zetu ndio mana sasa tunaingia katika agenda ya nishati safi ya kupikia wasimamizi ni sisi na nyinyi kwa hili” amesema kilangi.
Hata hivyo amefafanua kuwa kikao hicho kitawawezesha watendaji kupanga mpango mkakati wa mwaka mzima wa utekelezaji ikiwemo kufanya tafiti za mawimbi ya bahari ya kuzalisha umeme pamoja na kusambaza mtambo wa gesi kutoka bara.
Na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhandisi Felchesmi Mramba amesema jinsi ya kuendeleza mashirikiano kati ya Wizara hizo ni kuboresha huduma zinazotolewa naTaasisi hizo kwa Wananchi.
Hata hivyo ameeleza katika kikao hicho kutasaidia utekelezaji wa miradi ambayo inahusiana na taasisi hizo hasa kwenye takwimu za upepo wa umeme wa gesi kwa upande moja na kwa upande wa mafuta na gesi ili kuweza kuziratibu na kuzifanyia kazi.
Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamesema wataendeleza mashirikiano hayo kunufaika na vitu mbali mbali ikiwemo kubadilishana uzowefu wa kazi na kujua jinsi ya kutatua changamoto zinazojitokeza katika kazi zao sambamba na kutambua mifumo mbali mbali ya nishati pamoja na gesi.
Kikao hicho cha siku mbili ambacho kimewashirikisha wakurugenzi, watumishi maafisa mipango na wafanya kazi mbali mbali wanaoliomo ndani ya Taasisi zilizomo katika Wizara hizo.