Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Vikundi 37 vya Wanawake, Vijana na Wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro vimekidhi vigezo na kupatiwa mkopo wenye thamani ya shilingi Milioni mia moja themanini na moja na laki tano (181,500,000) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia program ya utoaji mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba inayosimamiwa na Halmashauri.
Kati ya vikundi hivyo 25 ni vya Wanawake ambapo wamenufaika na mkopo wa sh.129,500,000, vikundi 9 vya vijana vyenye jumla ya sh.36,500,000 na vikundi 3 vya watu wenye ulemavu vyenye jumla ya sh.15,500,000.
Akizungumza katika hafla fupi ya kugawa hundi kwa vikundi hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amewataka wanufaika kuhakikisha mkopo huo wautumie kwa shughuli iliyokusudiwa ili kukuza kipato na uchumi pamoja na kuzingatia kurejesha kwa mujibu wa mikataba yao.
“Namshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. @samia_suluhu_hassan, kuturejeshea fedha hizi kwenye Halmashauri zetu. Lakini pia @ortamisemi chini ya Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa uboreshaji wa kanuni za utoaji na urejeshaji wa fedha hizi ili zieendelee kuwa na tija kwa jamii”. Alisema DC Kasilda.
Pia amewapongeza Wanawake wa Same kwa kujitokeza kwa wingi kuchukua mikopo yenye masharti nafuu, ambapo wanufaika huanza kurejesha fedha miezi mitatu kuanzia tarehe ya kuchukua mkopo husika jambo ambalo huwezi kulikuta kwenye taasisi yeyote ya fedha.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Same Charles Anatoly amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 Halmashauri ya Same imetenga sh. 654,374,244.90 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu. Kwa robo ya kwanza (Julai hadi Septemba 2024) Halmashauri ilifungua dirisha la mikopo tarehe 23 septemba na lilifungwa tarehe 15 Oktoba 2024.