Mstahiki Meya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro Zuber Abdallah Kidumo amesema Mafunzo ya “Human Centred Design -HCD” ya Mchango mkubwa katika kutatua changamoto zinazoweza kukwamisha zoezi la chanjo .
Mhe. Kidumo amebainisha Hayo Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo ya HCD yanayolenga kushirikisha jamii kwa kutumia mbinu bunifu na Shirikishi katika kutatua changamoto zinazopelekea jamii kuwa na mtazamo hasi kuhusu umuhimu wa chanjo.
“Mafunzo kuhusu HCD yana umuhimu mkubwa kuwajengea uwezo Wananchi kutambua changamoto zinazowazuia kupata huduma za chanjo na kubuni mbinu Shirikishi na kuzitatua hivyo ushiriki wenu wa Mafunzo una tija kubwa katika kuibua changamoto na visababishi vinavyokwamisha wananchi kuwapeleka watoto kupata chanjo”amesema.
Kwa upande wake Simon Nzilibili kutoka Wizara ya Afya amesema Mafunzo ya HCD yanalenga kushirikisha jamii kwa kutumia njia bunifu huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kuwa na desturi ya kufuatilia mwenendo wa chanjo.
“Wazazi na walezi tuendelee kufuatilia mwenendo wa chanjo kwa watoto na Manispaa hii imefanya vizuri pia lengo la kufanya mafunzo hapa ni kujengeana uwezo ni mbinu gani ilitumia na kama kuna changamoto baadhi ya maeneo nini kifanyike” amesema.
Salome John Mwinjuma ni Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo chini ya Wizara ya Afya amesema katika kuimarisha Kinga ya mwili kwa mtoto mara tu anapozaliwa anatakiwa kupata chanjo.
“Mtoto anapozaliwa anatakiwa kupata chanjo katika kuimarisha Kinga “amesema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwajuma Nasombe amesema ni jukumu la kila mmoja kutoa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo huku akitoa wito kwa wadau kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali.
Mratibu wa chanjo Manispaa ya Moshi Upendo Shoo amesema mafanikio yaliyosaidia ni pamoja na uongozi imara, kutenga muda wa kukaa na timu kufuatilia takwimu sahihi na vikao vya kila wiki.
Dkt. Joseph Moshi ni Mkufunzi wa Mafunzo ya HCD amesema Mafunzo hayo yanamfikia hadi mlaji wa mwisho.