Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Desderius Haule na Makamu mwenyekiti Bahati Mbele kulia,wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Andrew Mbunda kushoto,kabla ya kuanza kwa kikao cha robo ya kwanza cha baraza la madiwani kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Andrew Mbunda(hayupo pichani)wakati akitoa taarifa mbalimbali kwenye kikao cha robo ya kwanza cha baraza la madiwani kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Desderius Haule,akifungua kikao cha Baraza la madaiwani kilichofanyika jana,kushoto kwake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Andrew Mbunda.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Andrew Mbunda ,akitoa taarifa ya mapato kwenye kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la madiwani ambapo Halmashauri hiyo imekusanya zaidi ya Sh.bilioni 2.9 katika kipindi cha miezi mitatu cha Julai-Septemba 2024katikati Mwenyekiti wa Halmashauri Desderius Haule.
…….
Na Mwandishi Maalum, Mbinga
HALMASHAURI ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,katika kipindi cha miezi mitatu Julai hadi Septemba 2024 imekusanya zaidi ya Sh.bilioni 2,964,142,561 sawa na asilimia 35 kati ya lengo la kukusanya Sh.bilioni 8,400,000,000 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Andrew Mbunda amesema hayo jana,kwenye kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Aidha alisema,hadi tarehe 30 Septemba Halmashauri imepokea Sh.bilioni 7,042,293,300 sawa na asilimia 26 ya makisio ya Sh.bilioni 27,227,634,000.00 kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Sh.bilioni 1,769,097,000 kati ya Sh.bilioni 2,536,195,000.00kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Alisema,ongezeko hilo ni baada ya kupokea Sh.bilioni 1,417,962,000.00 kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika tarehe 27 Novemba kwa ajili ya kuwapata viongozi wa vitongoji na vijiji.
Katika hatua nyingine Mbunda alisema, Halmashauri imepokea jumla ya Sh.bilioni 3,291,768,549 kati ya Sh.bilioni 9,918,358,720 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya wananchi waliopo katika Halmashauri hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kisale Makori,amewapongeza watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya Mbinga kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi na kusimamia shughuli za maendeleo ikiwemo zoezi la uandikishaji wananchi katika Daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Makori aliyewakilishwa na kaimu katibu tawala wa wilaya hiyo Karim Mzee,amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanachangia chakula kwa ajili ya watoto wao waliopo shuleni badala ya kazi ya kutoa chakula kuachwa ifanywe na Serikali.
Kwa upande wake Mwakilishi wa katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Amandus Chilumba,amewaasa madiwani wa Halmashauri ya wilaya kuendelea kudumisha upendo na mshikamano utakaosaidia Halmashauri yao kuwa kinara kwa kukusanya mapato ya ndani katika mkoa wa Ruvuma.
Alisema,Halmashauri itapata maendeleo iwapo kutakuwa na maelewano kati ya madiwani,wakuu wa idara na watumishi wa ngazi ya chini ambao kimsingi ndiyo wanaotumika katika kukusanya mapato na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Chilumba,amewataka watumishi wa Halmashauri kuwa wabunifu kwa kutafuta na kuibua vyanzo vipya vya mapato na kudhibiti mianya yote inayochangia kutoroshwa mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.
“Waheshimiwa madiwani suala la kukusanya mapato siyo mweka hazina pake yake,bali kila mmoja anawajibika katika kuibua vyanzo vipya,kukusanya na kudhibiti mapato yenu,nawaomba sana mshirikiane katika kazi hii”alisema Chilumba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mbina Desderius Haule,amewaomba madiwani kwenda kusimamia miradi inayotekelezwa katika kata zao ili iweze kukamilika kwa wakati na kuharakisha maendeleo kwa wananchi na wilaya ya Mbinga kwa ujumla.
Amemuagiza mweka hazina wa Halmashauri Samwel Marwa, kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa kutumia mashine za POS na kuwachukulia hatua watendaji watakaochezea mashine hizo.
Mweka hazina CPA Samweli Marwa alisema,wanazo mashine za POS zaidi ya 200 zinazotumika kukusanya mapato kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo kwenye mageti,hata hivyo amewaomba madiwani kushirikiana na idara ya fedha katika kukusanya mapato na wale wanaohitaji mashine hizo kwenda ofisini kwake.