Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ilulu Ilulu akionesha fedha ambazo zinatumika kwa sasa pamoja na fedha za zamani ambazo zinahitajika kuondolewa kwenye mzunguko wakati akiwa katika mkuano na waandishi wa habari uliofanyika leo Oktoba 31, 2024, Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ilulu Ilulu akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 31, 2024, Dar es Salaam kuhusu zoezi la kuondoa noti za zamani za shilingi ya Tanzania katika mzungumo wa fedha linalotarajiwa kuanza Januari 6, 2025 hadi April 5, 2025.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka watanzania kuziwasilisha noti za zamani za shilingi ya Tanzania katika ofisi za benki kuu pamoja na benki zote za biashara na kupatiwa malipo yenye thamani ya kiasi kitakachowasilishwa katika zoezi linalotarajiwa kuanza Januari 6, 2025 hadi April 5, 2025.
Hatua hiyo imekuja baada BoT kuanzia Januari 6, 2025 hadi April 5, 2025 wanatarajia kuanza zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani za shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1,000), elfu mbili (2,000), elfu tano (5,000), elfu kumi (10,000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi 2003 pamoja na noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Oktoba 31, 2024 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu BoT, Bw. Ilulu Ilulu, amesema kuwa baada ya April 5, 2025 mtu yoyote au taasisi itakayomiliki fedha hizo hazitaruhusiwa kutumika katika kufanya malipo sehemu yoyote Duniani.
Bw. Ilulu amesema kuwa wakati umefika kwa wananchi walioweka akiba ya noti za zamani kuzibadilisha au kuweka amana kwenye benki yoyote katika kipindi kilichotolewa.
“Kwa mantiki hiyo baada ya tarehe 5/4/2025 noti hizo zitakoma kuwa halali kwa malipo ya Tanzania na Duniani Kote” amesema Bw. Ilulu.
Amewataka watanzania wahakikishe wanakwenda kubadilisha noti tu zilizo halali zenye alama za usalama na faida ya kufanya hivyo ni kupata thamani ambayo walidhani imepotea.
Katika hatua nyengine amewataka watanzania kuacha kuuza na kukununua noti chakavu mitaani kwani ni kosa kisheria na kinachofanyika ni utapeli.
Amesema wananchi wanatakiwa kwenda kubadilisha noti hizo katika Benki za Biashara nchini kwani kuna madirisha maalumu ya kubadilishia fedha hizo.
“Naomba wananchi waende wenyewe kubadilisha fedha katika madirisha yaliyofunguliwa katika benki zote za biashara kunufaika na huduma hiyo” amesema Bw. Ilulu.