Na Ashrack Miraji – Fullshangwe Media
Timu ya vijana wa Stand kutoka Wilaya ya Same, Terminal FC, imetwaa kombe la MATHAYO CUP 2024 baada ya kuwafunga Manka FC kwa mabao 4-1. Manka FC, maarufu kama “wazee wa kuleta nyuki uwanjani,” walikutana na kipigo kikali katika fainali hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Kata ya Kisiwani, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro.
Mchezo huo ulihudhuriwa na mamia ya mashabiki kutoka kata mbalimbali ndani ya wilaya hiyo. Manka FC walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika za mwanzo, na kipindi cha kwanza kilimalizika kwa wao kuongoza 1-0. Hata hivyo, kipindi cha pili kiliashiria mwanzo wa mabadiliko makubwa, ambapo Terminal FC walifanikiwa kusawazisha bao hilo na kuwaduwaza wapinzani wao.
Dakika chache baadaye, Terminal FC waliongeza bao la pili na kuzima kelele za mashabiki wa Manka FC. Mabao mengine mawili yaliyofuata yalizidi kuzima matumaini ya Manka FC, na hadi mwisho wa mchezo, Terminal FC walikuwa na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Manka FC.
Baada ya mechi hiyo, mdhamini wa mashindano hayo, Mheshimiwa David Mathayo, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, alieleza kufurahishwa kwake na mwitikio wa wananchi wa Same, hususan Jimbo la Same Magharibi. Alisisitiza kuwa mashindano hayo yataendelea kwa lengo la kuibua vipaji vya soka na kutoa fursa za ajira kwa vijana wa jimbo hilo.
“Kwanza niwashukuru sana wananchi wa Same kwa kujitokeza kwa wingi sana uwanjani, na niwapongeze washindi wote kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa nne. Hongera nyingi kwa vijana wa Stand Same Terminal FC kwa kutwaa kombe la MATHAYO CUP. Hakika tumeona fainali yenye vipaji na ubunifu mkubwa mno katika soka,” alisema Mheshimiwa Mathayo.
Mheshimiwa Mathayo aliongeza kuwa msimu ujao zawadi kwa mshindi wa kwanza itapanda kutoka milioni 7 hadi milioni 10, akiwataka vijana kujiandaa na kuendelea kujifua ili kujitangaza kupitia mashindano haya.
Katika fainali hiyo, mshindi wa kwanza alijinyakulia kombe lenye thamani ya laki tano, pesa taslimu milioni 7, seti ya jezi, mpira, na medali kwa wachezaji na viongozi wa timu. Mshindi wa pili alipata milioni 5, jezi, mpira na medali, huku mshindi wa tatu akipata milioni 3.5, jezi, mpira, na medali. Mshindi wa nne alipewa kitita cha milioni 1.