Na Sophia Kingimali
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amewataka viongozi wa dini nchini kushirikiana na serikali katika kutoa elimu ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko kwa kutumia nyumba zao za ibada kuelimisha waumini kuhusu tahadhari za magonjwa hayo.
Dk. Mollel alitoa kauli hiyo leo, Oktoba 26, 2024, jijini Dar es Salaam, alipomuwakilisha Waziri wa Afya, Jenister Muhagama, katika kikao na viongozi wa dini. Kikao hicho kililenga kujadili tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko na suala la bima ya afya kwa wote.
“Kazi yenu kubwa sio tu kwamba mnao watu wengi, bali mmeushika ulimwengu, hivyo mnauwezo wa kuunganisha jamii. Tukiyumba katika suala la afya, uchumi pia utayumba,” alisema Dk. Mollel
Aidha, aliwataka viongozi hao kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kupambana na magonjwa hayo ili kuiwezesha Tanzania kuwa salama kwa kufuata kanuni za afya zinazotolewa na wataalamu.
“Rais Dk. Samia ametoa fedha na vifaa kuhakikisha maeneo ya mipakani wanadhibiti ugonjwa kabla ya kuingia nchini. Watanzania wawe na amani na waendelee kufanya shughuli zao kwa sababu Tanzania ni salama,” aliongeza Dk. Mollel
Alibainisha kuwa Tanzania bado haina magonjwa hayo ya mlipuko, ingawa nchi jirani zimeripoti maambukizi. Serikali inaendelea kuchukua tahadhari kuhakikisha magonjwa hayo hayafikii wananchi.
Kwa upande wao, viongozi wa dini wameahidi kushirikiana na serikali katika kutoa elimu ya magonjwa ya mlipuko kwa waumini wao kupitia nyumba zao za ibada.
Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ally Ngeruko, alishukuru serikali kwa ushirikiano mzuri na viongozi wa dini. “Rais Dk. Samia mara zote yupo karibu na viongozi wa dini kusimamia masuala ya kijamii, na sisi hatutamuangusha. Tutatoa elimu ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko kwa waumini wetu,” alisema Sheikh Ngeruko.
Askofu Gabriel Magwega, mwakilishi wa makanisa ya CCT, alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa waumini ili waweze kutambua dalili za magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, Marburg, na mpox, na kuwashauri kwenda haraka katika vituo vya afya kwa uchunguzi zaidi.
Naye, mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Sister Florida Bonifasi, alihimiza viongozi wenzake kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kwa waumini ipasavyo ili kudhibiti magonjwa hayo.