Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja akimkabidhi zawadi ya ushindi wa pili katika uandishi wa Insha kuhusu masuala ya fedha mwanafunzi Vivian Amwile Kalyoto kutoka shule ya sekondari Busokelo wilayani Rungwe mkoani Mbeya wakati wa kufunga maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kulia ni Meneja wa Uendeshaji wa DIB, Bw. Nkanwa Magina.
Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja akimkabidhi zawadi ya ushindi wa pili katika uandishi wa Insha kuhusu masuala ya fedha mwanafunzi Rachel Lucas Mwamalili wa shule sekondari Mbeya jinini MbeyaMbeya, kulia ni Meneja wa Uendeshaji wa DIB, Bw. Nkanwa Magina.
…………….
NA JOHN BUKUKU, MBEYA
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imewatoa hofu Watanzania kuhusu usalama wa matumizi ya huduma za kibenki katika shughuli za maendeleo, kwa kuwa na uhakika wa kinga ya amana iwapo benki itakumbwa na misukosuko ya kiuchumi.
Akizungumza leo Oktoba 26, 2024, katika Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Ruanda-Nzovwe jijini Mbeya, Meneja wa Uendeshaji wa DIB, Bw. Nkanwa Magina, alieleza kuwa jukumu la bodi hiyo ni kulinda amana za wateja katika benki na taasisi za fedha zinazotoa huduma za kibenki.
Magina alieleza kuwa, iwapo benki itapata changamoto za kiuchumi, mteja atakuwa na haki ya kulipwa fidia kati ya shilingi moja hadi shilingi milioni saba na laki tano.
“Majukumu yetu ni kutoa kinga dhidi ya upotevu wa sehemu au amana zote za wateja katika benki na taasisi za fedha pamoja na kuleta utulivu katika mfumo wa fedha nchini,” alisema Magina.
Aliongeza kuwa, katika maonesho hayo, Bodi ya Bima ya Amana imekuwa sehemu ya wadhamini na imewapatia zawadi wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliotoa mchango mzuri katika uandishi wa masuala ya kodi na bima ya amana.
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) ni taasisi iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha Na. 5 ya mwaka 2006, sehemu ya VII, kifungu cha 36 hadi 42, ikiwa na jukumu la kulinda amana za wateja katika taasisi za kifedha nchini Tanzania.
Katika hafla hiyo ya kufunga wiki ya Huduma za Fedha jinini Mbeya pia Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imetoa zawadi kwa washindi wa shindano la uandishi wa insha kwenye Maadhimisho hayo ambapo Shindano hilo lililenga kuhamasisha na kutoa elimu kwa vijana kuhusu umuhimu wa bima ya amana na nafasi yake katika kuimarisha mfumo wa kifedha nchini Tanzania.
Wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari walishiriki katika shindano hilo, wakiandika insha zinazohusiana na mada ya bima ya amana na jinsi inavyolinda amana za wateja katika benki na taasisi za kifedha. Wanafunzi waliofanya vizuri walitunukiwa zawadi zikiwemo vifaa vya shule na vikombe, kama njia ya kuwapongeza na kuwawezesha kuendeleza masomo yao.
Akizungumzia zawadi hizo Bw. Nkanwa Magina, alisema kuwa utoaji wa zawadi kwa wanafunzi hao ni sehemu ya mikakati ya bodi hiyo ya kueneza uelewa juu ya umuhimu wa bima ya amana. Alisema kuwa Bodi ya Bima ya Amana inatambua mchango wa vijana katika kujenga jamii yenye elimu ya kifedha, na hivyo imejikita katika kutoa fursa kama hizi ili kuwasaidia kujifunza kuhusu masuala ya kifedha mapema.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa mwaka huu yana kaulimbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi.” Bodi ya Bima ya Amana ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki katika kutoa elimu kwa wananchi, huku ikiwahamasisha Watanzania kufahamu haki zao kama wateja wa huduma za benki na namna ya kuhakikisha usalama wa amana zao.
Meneja wa Uendeshaji wa DIB, Bw. Nkanwa Magina akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo kwa wanafunzi walioshinda Shindano la uandishi wa Insha kuhusu masuala ya fedha.