…………………..
Na Sixmund Begashe – Rubondo Geita
Wananchi wametakiwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika ulinzi wa maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ili maliasili hizo ziweze kuwanufaisha watanzania wote badala ya kuwanufaisha watu wachache wenye uchu wa mali na wanaofanya uharibifu ikiwemo uwindaji haramu, kukata na kuchoma moto misitu na kuendesha shughuli za kilimo Hifadhini jambo linalosababisha changamoyo ya wanyamapori wakali na wahariibifu.
Akizungumza katika Hifadhi ya Taifa Rubondo Mkoani Geita wakati wa kuhitimisha ziara yake aliyoifanya Mikoa ya Simiyu, Mara, Mwanza na Geita kwa lengo la kukagua shughuli za uhifadhi na kuzungumza na Kuu za Wilaya za Mkoa wa Simiyu, Maasifa wa Jeshi la Uhifadhi pamoja na Askari wake.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba amesema changamoyo iliyopo ya Wanyamapori wakali na waharibifu inaendelea kushughulikiwa kikamilifu na Wizara hiyo.
“Tunafahamu yakuwa suala la uhifadhi ni suala muhimu kitaifa na kimataifa kwa sababu hiyo, Wizara itaendelea na majukumu yake ya uhifadhi, wakati huo huo tukiendelea kuangalia namna ya kushirkiana na Wizara zingine za kisekta ili kuwezesha shughuli za kijamii kufanyika bila kuathiri shughuli za uhifadhi”. Alisema na kufafanua CP. Wakulyamba
CP. Wakulyamba ameongeza kuwa, kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii wataendelea kuongeza juhudi za kuisimamia nidhamu kwa askari wa Jeshi hilo, kuimarisha ulinzi wa kutosha katika maeneo ya Hifadhi ili wananchi wafanye shughuli zao kwenye maeneo yaliyoruhusiwa kisheria kwa usalama na Hifadhi ziendelee kutoa huduma katika maeneo yao.
“Katika suala la kuliimarisha Jeshi la Uhifadhi, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele kuendeleza utalii na kuvijengea uwezo vyombo vya ulinzi hususani Jeshi letu la Uhifadhi ili kuwa Jeshi imara linalofanya kazi kwa kuzingatia Misingi ya haki za Binadamu na utawala bora” Alisisitiza CP. Wakulyamba
Ziara hiyo ililenga kutekeleza Maagizo ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyotokana na Maoni ya Tume ya Haki Jinai ya kuboresha Jeshi hilo kwa kutoa Mafunzo yakuwawezesha kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Misingi ya Sheria na Haki za Binadamu.
Ziara hii ya Naibu katibu Mkuu Maliasili pia lilenga kufuatilia utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu wa CCM Mh. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi aliyolitoa kwenye Ziara yake Mkoani Simiyu juu ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu. Aidha, Wizara imeahidi kutekeleza maelekezo hayo, ikiwemo kuongeza nguvu ya kudhiti wanyamapori wakali na waharibifu na kutoa elimu kwa wananchi ya kujikinga na madhara ya wanyama hao.