Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika leo Oktoba 24, 2024 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii.
Afisa Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Alex Nelson Malanga akizungumza jambo katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika leo Oktoba 24, 2024 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Jane Mihanji akizungumza jambo katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika leo Oktoba 24, 2024 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii.
………….
NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Tume ya Madini Tanzania imefanikiwa kupiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka mitano baada ya kufanikisha makusanyo ya maduhuli kutoka shilingi bilioni 624.6 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 753.8 kwa mwaka 2023/2024.
Akizungumza leo Oktoba 24, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema kuwa lengo la makusanyo kwa mwaka 2024/2025 ni kufikia shilingi trilioni moja sawa na wastani wa kukusanya shilingi bilioni 83.33 kila mwezi.
Mhandisi Lwamo amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 257.89 zimekusanywa, huku akieleza kuwa makusanyo hayo ni sawa na asilimia 103.16 ya lengo kwa kipindi husika, ambapo sawa na asilimia 25.79 ya lengo la mwaka 2024/2025.
“Tumefanikio hayo yametokana na kuimarisha mazingira ya utendaji kazi wa Tume ya Madini, usimamizi wa sekta ya madini na ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini” amesema Mhandisi Lwamo.
Mhandisi Lwamo ameeleza kuwa wanaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa pamoja na kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi kunufaika na rasilimali madini.
Amesema kuwa miongoni mwa vipaombele vya Tume ya Madini ni kuendelea kuelimisha umma na kuboresha mawasiliano kati ya Tume na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya madini na kuendeleza rasilimali watu.
Mhandisi Lwamo amefafanua kuwa ukuaji wa mchango wa seka ya madini (GDP) 9 kwa mwaka 2023, huku mauzo ya madini yameongezeka kutoka shilingi bilioni 2,361.80 kwa mwaka 2021/22 hadi kufikia shilingi bilioni 956.76 kwa mwaka 2024/25.
Amesema kuwa pia bidhaa zenye thamani ya USD bilioni 3.78 ziliuzwa migodini, huku kampuni za watanzania ziliuza bidhaa zenye thamani ya USD bilioni 3.46 (91.68%) na wageni waliuza USD bilioni 0.31 (8.32%).
“Tumefanya uwezeshaji kwa wachimbaji wadogo 867,124 kwa kutoa elimu ya ugani kuhusu usalama, afya, mazingira, pamoja na usimamizi wa baruti ili kuwa na uchimbaji salama na endelevu” amesema Mhandisi Lwamo.
Amesema kuwa ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima wamefanikiwa kutenga maeneo yenye tija kwa ajili ya shughuli za uchimbaji ambapo hadi sasa jumla ya maeneo 58 yametengwa.
“Tumewaunganisha wachimbaji wadogo na Taasisi za Kifedha ili waweze kuongeza mitaji yao katika shughuli za uchimbaji” amesema Mhandisi Lwamo.
Ameeleza kuwa mikakati ya tume ya madili iliyopo kwa sasa ni pamoja na kuongeza mapato na kuimarisha uchimbaji endelevu, kupungua kwa matukio ya utoroshaji wa madini pamoja na kupunguza migogoro itokanayo na muingiliano wa maombi ya leseni
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Jane Mihanji ametoa wito kwa Tume ya Madini kuwa na utaratibu wa kufanya kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari ili kutoa fursa ya kuendelea kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali yanaendelea katika sekta ya madini.
Tume ya Madini ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Madini iliyoanzishwa Mwaka 2017 chini ya Sheria ya Madini Sura 123 ikiwa na jukumu la kusimamia shughuli zote zinazohusiana na madini nchini kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 22 cha Sheria ya Madini.
Tume ya Madini inasimamiwa na Tume yenye Mwenyekiti na Makamishna nane, katika utendaji wa kila siku Tume inaongozwa na Katibu Mtendaji, anayesaidiwa na Wakurugenzi 7 na Maafisa Madini wa Mikoa ya Kimadini 30.